Nilifikiria kupunguza uzito na kupata pesa nyingi nitapata furaha - Chebet Rono

Rono alisema kuwa alikuwa akifikiriakwamba kupata pesa nyingi na kupunguza uzito kutamponya kutoka kwa aliyokuwa anapitia kumbe sivyo.

Muhtasari

• “Mara nyingi tunafikiri tuna maisha ya kuishi lakini hatujui siku tunayoondoka kwa hivyo ninaishi kila siku kama ni mwisho wangu!" - Rono.

Chebet Rono azungumzia safari yake ya kupunguza uzito.
Chebet Rono azungumzia safari yake ya kupunguza uzito.
Image: Instagram

Mwanablogu Chebet Rono amefunguka jinsi alikuwa anadhani kushiriki mazoezi ya kupunguza uzito wa mwili na kutengeneza pesa nyingi kungemtoa katika matatizo ya yale yote ambayo alikuwa anapitia.

Rono kupitia Instagram yake, alipakia picha tofauti zikimuonesha kabla na baada ya kushiriki mazoezi ya kupunguza uzito wa mwili na kusema kuwa katika fikira zake alikuwa anadhani akipata muonekano mzuri wa mwili ndio ungekuwa mwisho wa madhira yake.

Lakini sivyo, Rono ambaye anaonekana kujuta na pengine kusumbuliwa na unyongovu alisema kuwa bado kuna mambo mengi tu anazidi kung’an’ana nayo na ambayo yamemuumiza sana nafsi yake.

“Nakumbuka nikifikiria kwamba ikiwa hatimaye nitapunguza uzito na kupata pesa zaidi nitafurahi na kuponywa kutoka kwa kila kitu nilichopitia. Kwamba sitawahi kujishuku au kuhisi hofu au kujihujumu tena vizuri. Haifanyi kazi kama hiyo kwa YOTE nilikuwa na kile nilichotaka lakini bado nilirudia mizunguko ile ile,” Rono alisema kwa kujuta.

Rono alisema kuwa amejifunza kitu kimoja kwamba kupata uponyaji wa kipekee ni kujikubali jinsi ulivyo na wala si kufanya jinsi watu wanakutaka ufanye.

“Na nikagundua uponyaji na kukua sio kile tunachotarajia ni kuchagua mwenyewe hata unapojishusha na kukabiliana na mapepo yako tena na tena hadi yamekupita. Hivi majuzi nimekuwa na siku bora zaidi za maisha yangu kwani niliacha mambo mengi ambayo siwezi kudhibiti na kuwapo iwezekanavyo, nikichukua wakati mwingi kunusa waridi tukiwa bado hapa.”

“Mara nyingi tunafikiri tuna maisha ya kuishi lakini hatujui siku tunayoondoka kwa hivyo ninaishi kila siku kama ni mwisho wangu! Hapa ni kusawazisha na kujiamini,” Rono alisema.