Diaomond Platnumz apata kazi serikalini nchini Tanzania

Diamond aliteuliwa kwa kigezo cha kuwa na ufuasi mkubwa Instagram, kwa imani kwamba ujumbe wake utawafikia watu wengi chini ya sekunde moja.

Muhtasari

• Diamond Platnumz aliteuliwa kuwakilisha vijana wa kiume kwenye baraza hilo la kiserikali huku Shilole akiwakilisha vijana wa kike.

Diamond Platnumz apewa kazi serikalini TAanzania.
Diamond Platnumz apewa kazi serikalini TAanzania.
Image: Instagram

Msanii namba moja wa muda wote katika ukanda wa Afrika Mashariki Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz rasmi amepata kazi katika serikali ya Tanzania.

Katika tangazo ambalo lilitangazwa alasiri ya Jumanne, Diamond Platnumz ni miongoni mwa watu maarufu ambao waliteuliwa kama wawakilishi wa vijana katika bodi ya kupambana na ugonjwa wa Malaria.

“Kama unavyofahamu katika kila watu 100 nchini Tanzania, watu 77 wana umri chini ya miaka 35. Asilimia 77 ya Watanzania ni vijana. Imempendeza mheshimiwa rais kumteua Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz kuwa mwakilishi wa vijana katika baraza la kitaifa la kutokomeza malaria akiwakilisha wasanii wa kiume,” sehemu ya taarifa hiyo iliyosomwa na mwakilishi wa rais alisema.

Si tu Diamond ambaye alipata uteuzi huo, wasanii wengine pia walifaidi kutokana na uteuzi huo wa rais ambapo kwa upande wa wasanii wa kike, msanii ambaye pia ni mwigizaji Shilole aliteuliwa kufanya kazi sambamba na Diamond kwenye baraza hilo kama mjumbe wa baraza hilo.

Rais Samia alitetea uteuzi wa Diamond akisema kuwa kigezo kikubwa waliangalia ni ufuasi wake kwenye Instagram.

“Ana followers milioni 15.9 kwenye Instagram. Kwa hiyo akiandika tu ‘sio kila homa ni malaria’ inawafikia watu wengi ndani ya sekunde moja,” taarifa yake ilisema.

Kwa upande wa Shilole ambaye kando na kazi ya usanii pia ni mjasiriamali wa mgahawa wa Shsishi Foods ana wafuasi milioni 9, jambo ambalo walisema linaweza kufanikisha ujumbe wa kutoa hamasa dhidi ya Malaria kuwafikia watu wengi kwa muda mchache.

Nchini Kenya, wiki chache zilizopita uteuzi kama huo ulifanywa katika wizara ya maswala ya vijana, sanaa na michezo ambapo wasanii wengi maarufu tu walijinafasi katika nyadhifa mbalimbali serikalini.

Wasanii kama vile Akothee, Wahu ni miongoni mwa walioramba dili nono la kufanya kazi kwenye baraza la kuzingatia kazi za sanaa chini ya waziri Ababu Namwamba.