Watu wafurika kuomba Diamond neti za mbu baada ya kupata kazi baraza la kumaliza Malaria

Diamond alisema pindi baada ya kutangazwa kuwa mwanachana wa baraza hilo, tayari amepokea maombi kadha watu wakitaka vyandarua.

Muhtasari

• Rais Samia alitetea uteuzi wa Diamond akisema kuwa kigezo kikubwa waliangalia ni ufuasi wake kwenye Instagram.

• Diamond atakuwa mwakilishi wa vijana wa kiume kwenye baraza hilo la kupambana na Malaria nchini Tanzania.

Diamond alalamika maombi mengi ya vyandarua baada ya kuteuliwa baraza la kupambana na malaria.
Diamond alalamika maombi mengi ya vyandarua baada ya kuteuliwa baraza la kupambana na malaria.
Image: Instagram

Siku moja tu baada ya mjumbe wa rais Samia Suluhu Hassan kuweka wazi kwamba msanii Diamond Platnumz ni mmoja wa wanachama wateule katika baraza la kitaifa la kupambana na Malaria, msanii huyo amedokeza kuwa mamia ya watu wamemsakama kwenye koo wakimuomba kuwapa vyandarua vya kujikinga dhidi ya mbu.

Diamond kupitia ukurasa wake wa Twitter alisema kuwa tayari hata kabla ya saa 24 kupita tangu uteuzi wake kuwekwa wazi, ameshapokea maombi kadha wa kadha kutoka kwa watu ambao wanamtaka kuwafanyia mradi wa kupata vyandarua hivyo.

Msanii huyo alisema kuwa maombi hayo ni mengi na kutania kuwa watu watamuua kwa kuweka maombi hayo kwani ndio mwanzo ameteuliwa hata ofisini hajafika.

“Jamani mtaniua na haya maombi yenu ya Vyandarua, uteuzi wenyewe ndio kwanza mpya 😅” Diamond aliandika.

Katika tangazo ambalo lilitangazwa alasiri ya Jumanne, Diamond Platnumz ni miongoni mwa watu maarufu ambao waliteuliwa kama wawakilishi wa vijana katika bodi ya kupambana na ugonjwa wa Malaria.

“Kama unavyofahamu katika kila watu 100 nchini Tanzania, watu 77 wana umri chini ya miaka 35. Asilimia 77 ya Watanzania ni vijana. Imempendeza mheshimiwa rais kumteua Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz kuwa mwakilishi wa vijana katika baraza la kitaifa la kutokomeza malaria akiwakilisha wasanii wa kiume,” sehemu ya taarifa hiyo iliyosomwa na mwakilishi wa rais alisema.

Si tu Diamond ambaye alipata uteuzi huo, wasanii wengine pia walifaidi kutokana na uteuzi huo wa rais ambapo kwa upande wa wasanii wa kike, msanii ambaye pia ni mwigizaji Shilole aliteuliwa kufanya kazi sambamba na Diamond kwenye baraza hilo kama mjumbe wa baraza hilo.

Rais Samia alitetea uteuzi wa Diamond akisema kuwa kigezo kikubwa waliangalia ni ufuasi wake kwenye Instagram.