Mwanahabari nguli wa Kiswahili Salim Kikeke aondoka BBC baada ya miaka 20

“Ni muhimu kufahamu wakati sahihi wa kuteua. Binadamu tumeumbwa na miguu ili tutembee." - Kikeke alisema.

Muhtasari

• "Nimesimama hapa kwa takribani muongo mmoja na nadhani ni wakati mwafaka wa kutembea" - Kikeke.

Salim Kikeke aondoka BBC baada ya miaka 20.
Salim Kikeke aondoka BBC baada ya miaka 20.
Image: Facebook

Mwanahabari mahiri wa Kiswahili kutoka Tanzania amefanya shoo yake y mwisho katika idhaa ya habari ya BBC huko London Uongereza usiku wa Ijumaa.

Kikeke alitangaza kwamba atakuwa anaondoka katika idhaa hiyo ya habari za dunia, baada ya kuifanyia kazi kwa miaka 20.

Kikeke baada ya kumaliza kuwasilisha habari za Dira ya Dunia Aprili 28, aliweka wazi kwamba ndicho kibarua chake cha mwisho katika idhaa hiyo huku akikumbuka jinsi alivyoanza kazi katika BBC mwaka 2003.

“Leo ni siku yangu ya mwisho kama mtangazaji kinara wa BBC idhaa ya Kiswahili. Nimekuwa BBC kwa miaka 20, kumi nikiwa kama mtangazaji wa redio na mhariri wa tovuti yetu ya BBC Swahili na miaka mingine kumi kama kinara wa dira ya dunia kwenye TV,” Kikeke alianza.

Hata hivyo, Kikeke aliweka wazi kwamba hakufutwa kazi bali ni kuondoka tu kwa ridhaa yake kwani wakati mwingine kukaa mahali pamoja kwa muda mrefu unaweza ukaharibu na ni sharti ujue muda wa kuondoka.

“Ni muhimu kufahamu wakati sahihi wa kuteua. Binadamu tumeumbwa na miguu ili tutembee. Nimesimama hapa kwa takribani muongo mmoja na nadhani ni wakati mwafaka wa kutembea na isingekuwa vyema kuondoka kimya kimya, niko hapa leo kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mungu ambaye ameniwezesha kufika hapa lakini pia kwako wewe ambaye umekuwa ukitufuatilia katika TV na redio…” Kikeke alisema huku machozi ya furaha yakimlengalenga.

Kikeke hakufichua kituo chake kinachofuata lakini alidokeza "kuwa karibu". Alifichua kwamba angekosa mazingira ya BBC ambayo alifanya kazi na wenzake wazuri ambao alifanya nao kazi.