Baada ya miaka 25, Gidi akutana na rafiki Msudani waliyesoma na kulala naye shuleni

"Ilikuwa mkutano wa kihisia tulipokumbuka jinsi tulivyokuwa tukilala sakafuni na kuweka chakula baridi cha mchana kwa chakula cha jioni." - Gidi.

Muhtasari

• "Nilikuwa nikikosa karo ya shule na nauli ya kila siku ya basi kwenda na kurudi Dandora" - Gidi alikumbuka.

• Mtangazaji huyo alifichua kwa furaha kwamba miaka 25 baadae, rafiki yake ni afisa mkuu katika setikali ya Sudani Kusini.

Gidi afurahia kukutana na rafiki wa shuleni baada ya miaka 25
Gidi afurahia kukutana na rafiki wa shuleni baada ya miaka 25
Image: Facebook//Joe Gidi

Mtangazaji wa redio Jambo Joe Gidi alishindwa kuficha furaha yake baada ya kukutana na rafiki wake raia wa Sudani Kusini waliyekuwa wakisoma naye shule ya upili miaka 25 iliyopita.

Gidi aliibua kumbukumbu jinsi walivyokutana na Msudani huyo na kuishia kuwa Zaidi ya marafiki kutoka kusoma pamoja, kula na hadi kulala pamoja katika chumba kilichotengwa kama bweni mbadala kwa wanafunzi ambao walikuwa wanatoka mbali na hawakuwa na nauli ya kusafiri kurudi nyumbani kutoka shuleni.

“Sehemu ya shida zaidi ya maisha yangu ilikuwa katika shule ya upili katika Shule ya Upili ya Aquinas AKA AQ. Nilikuwa nikikosa karo ya shule na nauli ya kila siku ya basi kwenda na kurudi Dandora, kwani AQ ilikuwa shule ya kutwa. Sikuwa peke yangu, tulikuwa na Wasudan kadhaa wa kusini ambao pia walikosa nauli,” Joe alikumbuka.

Mtangazaji huyo aliyesherehekewa Zaidi kwa weledi wake nyuma ya kipaza sauti studioni alisema kuwa shule hiyo ya kutwa ilijipata ikigeuzwa kuwa ya bweni baada ya mwalimu mkuu kuwataka wanafunzi waliokuwa wakitoka mbali kuanza kukaa kule.

“Siku moja mkuu wetu wa shule Bw KK Kingori alipendekeza kwamba wale ambao hawakuweza kumudu nauli ya kuja shuleni kila siku wanaweza kulala kwenye chumba cha kubadilishia nguo. Hivyo ndivyo bweni la AQ lilivyoanza na hivyo ndivyo nilivyojikuta na Wasudan Kusini 3 tukiwa na vyumba katika chumba cha kubadilishia nguo za michezo cha shule,” Gidi alikumbuka.

Mtangazaji huyo alifichua kwamba katika ‘bweni’ hilo ndiko ndoto yao ya kuwa wanamuziki ilizaliwa.

Na miaka 25 baadae, Gidi alijawa na furaha kukutana na rafiki wake mmoja kati ya hao watatu ambaye kwa sasa ni afisa mkuu katika serikali ya Sudani Kusini.

“Hapo ndipo nilipoanza kazi yangu ya muziki. Leo nimekutana na mmoja wao, Agel Machar ambaye sasa ni afisa mkuu wa Serikali katika Serikali ya Sudan Kusini, kwa mkutano baada ya miaka 25. Ilikuwa mkutano wa kihisia tulipokumbuka jinsi tulivyokuwa tukilala sakafuni na kuweka chakula baridi cha mchana kwa chakula cha jioni. Ninakupongeza Bw Machar, tumefika. Mungu aendelee kukubariki,” Gidi alisema kwa furaha.