Khaligraph, Nadia wamlipua Eric Omondi kisa video ghali ya shilingi milioni 3.8

"Wewe ndio utafanya wanablogu wenzako watozwe ushuru kwa sababu unabadilika katika harakati zako leo unasema hiki kesho unazungumza na rais kama mcheshi mwenzako."

Muhtasari

• Msanii huyo alitoa kauli hiyo siku moja tu baada ya kuichana serikali kwa kuja na mswada wa kifedha ambao unanuiwa kupitishwa bungeni na kuwa sheria.

Khaligraph Jones na Nadia Mukami wamlipua Eric Omondi kwa maamshi ya kebehi dhidi ya wasanii wa Kenya.
Khaligraph Jones na Nadia Mukami wamlipua Eric Omondi kwa maamshi ya kebehi dhidi ya wasanii wa Kenya.
Image: Screengrab

Msanii Eric Omondi kwa mara nyingine ameotesha upya ugomvi wake wa kibabe dhidi ya wasanii wa Kenya baada ya kutangaza kwamba Ijumaa hii ataachia video ya wimbo ambayo ilimgharimu kiasi kikubwa cha pesa.

Mchekeshaji huyo aliyegeuka kuwa mwanaharakati kupitia Instagram yake alipakia kipande kifupi cha video wakiwa na mwanasosholaiti Amber Ray na kudokeza kwamba ilimgharimu shilingi milioni 3.8 za Kenya.

Omondi katika kile kilionekana ni kutupa mkwara mzito kwa wasanii wa humu nchini ambao ameishi kuwataja kuwa wamekosa ubunifu, alisema kuwa video hiyo itakuwa kama funzo kwa wasanii kujua jinsi video hiyo inavyofanywa.

“Hii ilikuwa ni Picha tu!!! Tumefanya Video ya Muziki ya Ksh 3.8 Milioni ili tu kuwaonyesha Wasanii jinsi inavyopaswa kufanywa. Wimbo/Video ya Muziki itashuka IJUMAA SAA 10 AM!!!” Eric Omondi alisema.

Msanii huyo alitoa kauli hiyo siku moja tu baada ya kuichana serikali kwa kuja na mswada wa kifedha ambao unanuiwa kupitishwa bungeni na kuwa sheria.

Mswada huo ambao umekuwa ukisukumwa kwa Zaidi na viongozi wanaoegemea serikali unataka kuwekwa tozo ya asilimia 15 kwa wanablogu wa mitandaoni lakiji pia katika tozo ya asilimia tatu kwa ajili ya kile Ruto na serikali yake wanasema ni ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Hata hivyo baada ya kuonekana kuelekeza mshale wake kwa wasanii wa Kenya, wasanii hao hawakuachwa nyuma katika kujibu mipigo ambapo Khaligraph Jones alimtaka kuelekeza harakati zake katika jambo moja ili wajue kuwa anamaanisha.

“Unafaa kuchagua vita moja kaka ndio tujue unamaanisha. Jana ulikuwa unazungumzia suala nyeti ambalo lilinifanya nielekee kwenye studio ili kufanya ngoma lakini leo hii tena umeingia katika kufukuzia kiki. Halafu kesho tena utamzungumzia rais kama mcheshi mwenzako. Wewe ndio utafanya wanablogu kutozwa,” Khaligraph alimwambia.

Nadia Mukami pia alionekana kuungana na Jones akimsuta Omondi kubadilika kila mara katika kile anachokizungumzia na hivyo kuifanya iwe vigumu kwa watu kumchukulia kwa umakini katika harakati zake za kile anaita ni ukombozi wa vijana.