DJ Fatxo ajitupa mzima mzima kwenye uigizaji wa filamu

Fatxo anatangaza haya wiki chache baada ya sakata liilomhusisha na kifo cha Mwathi kuonekana kutokomea.

Muhtasari

• Msanii huyo aliyepigwa vita Zaidi mitandaoni tangu mwezi Februari alichukua pia nafasi hiyo kutoa shukrani zake kwa waliompigia kura kupelekea kushinda tuzo ya Msanii bora wa Mugithi.

DJ Fatxo ajitupa kwenye uigizaji wa filamu.
DJ Fatxo ajitupa kwenye uigizaji wa filamu.
Image: Instagram

Msanii wa Mugithi ambaye pia ni mcheza santuri, DJ Fatxo ametangaza ujio wake mpya safari hii si kwenye muziki bali katika tasnia ya kuigiza filamu.

Fatxo ambaye pia alitangaza kuachia wimbo wake wa kwanza kabisa baada ya kimya cha takribani miezi mitatu kufuatia sakata la kifo cha Jeff Mwathi alitangaza kuwa ataachilia filamu yake ya kwanza Juni 6 majira ya asubuhi na kuwataka mashabiki wake wa muda wote kutoachwa nyumba katika suala zima la kumpa sapoti.

“Sasa watu wa sinema mjiandae nakuja hiyo tasnia. Filamu yangu ya kwanza itashuka kesho san ne asubuhi,” aliandika Jumatatu alasiri.

Msanii huyo aliyepigwa vita Zaidi mitandaoni tangu mwezi Februari alichukua pia nafasi hiyo kutoa shukrani zake kwa waliompigia kura kupelekea kushinda tuzo ya Msanii bora wa Mugithi katika kitengo cha wanaume kwenye tuzo za E360.

Fatxo alishinda tuzo hizo mwezi Machi, lakini kipindi hicho hakuwa mitandaoni kutokana na zogo hilo ambalo wengi wa watu walikuwa wanamtuhumu kwamba alihusika katika kifo cha mbunifu Jeff Mwathi ambaye alisemekana kufariki baada ya kuanguka kutoka orofa ya 10 ya chumba ambacho Fatxo alikuwa anaishi mtaani Kasarani.

“Huwa naamini kuwa wakati mwingine nyakati mbaya katika maisha yetu hutuweka kwenye njia ya moja kwa moja ya nyakati bora zaidi za maisha yetu. Asante sana kwa kuniamini na kunipigia kura kama Msanii wa E360 Mugithi wa mwaka wa 2023 katikati ya fujo na hullabaloo. Hili tuzo ni letu sote,” Fatxo aliandika.

Msanii huyo Jumatatu pia alizua maswali mengi kuliko majibu baada ya kupakia klipu fupi akionekana na gari la zamani aina ya Toyota Corolla wakati wengi wamekuwa wakimzoea kumuona na gari la kifahari aina ya Mercedes.

Katika klipu hiyo, Fatxo alidokeza kuwa ndio mwanzo mpya na kuwaomba mashabiki wake kuzidi kumweka katika maombi kwani vita anayopigana bado haijakamilika japo inaonekana kutulia baada ya DPP kumuondolea mashtaka ya kumhusisha na kifo cha Mwathi.