Mwaka mmoja baadae! Karen Nyamu akumbuka kuvishwa kofia na Ruto

Nyamu alisema kuwa kipindi hicho na hata sasa wimbi la kisiasa bado linampendelea Ruto na alikuwa akikuvisha kofia hivi unajua uko mboni kushinda uchaguzi.

Muhtasari

• Ruto alikuwa anaendesha shughuli nyingi za kisiasa katika makazi rasmi ya naibu rais mtaani Karen, ambapo wanasiasa wengi walikuwa wanasajiliwa UDA kule.

Karen Nyamu akumbuka jinsi Ruto alivyomvisha kofia ya UDA
Karen Nyamu akumbuka jinsi Ruto alivyomvisha kofia ya UDA
Image: Instagam

Seneta maalum Karen Nyamu amerudisha wakenya nyuma kwa kumbukumbu wakati alijitupa nyuma ya rais William Ruto wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Nyamu ambaye ni seneta maalum wa chama cha UDA alipakia picha za kipindi hicho akimtembelea Ruto, waakti huo akiwa kama naibu wa rais na ambaye shughuli zake nyingi alikuwa anazifanya kutoka kwa nyumba ya makaazi ya naibu wa rais mtaani Karen.

Nyamu, kama wanasiasa wengine ambao walikuwa wanatawazwa na Ruto kwa kuvalishwa kofia maarufu ya UDA kila walipokwenda kwake Karen kutangaza rasmi kumuunga mkono katika azma yake ya urais, alisema kuwa anakumbuka vizuri sana jinsi matukio yalivyokuwa.

Alisema kuwa mtu yeyote ambaye alikuwa anavalishwa kofia na Ruto alikuwa anajua kwamba yuko angalau mbioni kushinda uchaguzi kwa wadhifa wowote wa kisiasa ambao angesimama, ilmradi tu alikuwa amesimama kwa tikiti ya chama cha UDA, kwani kipindi hicho asilimia kubwa ya wimbi la kisiasa ilikuwa inavuma kwa upendeleo wa Ruto kuibuka kuwa rais.

Nyamu wakati huo alikuwa ametangaza azma ya kuwania useneta Nairobi kwa tikiti ya UDA lakini baadaye kufuatia mashauriano ya ndani ya chama, alilazimika kusonga kando na kumuachia Askofu Margret Wanjiru kupeperusha bendera ya UDA katika useneta Nairobi – hata hivyo alipoteza kwake Edwin Sifuna aliyekuwa anawania kwa tikiti ya ODM.

“Ulikua ukivalishwa kofia unajua you’re halfway there to getting elected 😄😄 Ground ilikuwa na bado ni Rutonated!” Nyamu alisema.

Mwanasiasa huyo mwenye vimbwanga aliwahakikishia na kuwatoa wasiwasi wananchi kwamba wimbi la kisiasa bado liko upande wa Ruto, licha ya wengi wa waliomchangua kuonekana kwenda kinyume kwa kile wanasema kuwa mkuu wa taifa ameonekana kukiuka mengi ya aliyoahidi katika manifesto yake.