KRG afichua kwa nini alimchangia Mustafa 20k licha ya kuwa yeye ni bilionea

"Nilikuta kama wamechangisha pesa nyingi na zilikuwa zimesalia elfu 20 tu sasa mimi nikasema si nimalizie kujaza hiki kikapu," - KRG.

Muhtasari

• KRG aimlaumu Mustafa kwa kuteseka bila kusema, na kudai kuwa hawakuwa wanajua licha ya kwamba walikuwa marafiki.

KRG the Don
KRG the Don
Image: maktaba

Miezi miwili baada ya msanii Colonel Mustafa kuchangiwa na wasanii na wakenya mbalimbali wenye moyo safi, kulikuwa na sekeseke za ndani baada ya orodha ya majina ya wasanii maarufu kuvujishwa ikionyesha kiwango cha michango yao.

Wengi walishangaa ni kwa nini msanii KRG the Don aliamua kuchangia kiasi cha shilingi elfu 20 pekee licha ya kujidai na kujitapa kila kona kuwa yeye ni tajiri na msanii peke mweney thamani ya ubilionea.

Sasa msanii huyo amejitokeza wazi kuzungumzia hilo, akielezea ni kwa nini aliamua kutoa kiwango hicho kama wengi wa wasanii.

KRG alisema kuwa aliungwa kwenye lile kundi kuchelewa na alikuta tayari wasani wengi wameshachangisha kiasi kikubwa cha pesa karibia kufikia kiwango ambacho kilikuwa kimelengwa.

“Mimi waliniweka kwenye lile kundi mwisho kabisa. Nilikuta kama tayari wameshachangisha pesa na walikuwa wameweka lengo lao ni laki saba. Nilikuta wamechangisha tayari elfu 680. Nikakuta imesalia elfu 20 nikasema si nizime hili pengo,” KRG alisema.

Msanii huyo alisema kuwa maadui zake wa mitandaoni ndio walivujisha hiyo picha wakilenga kumchafulia jina kwamba hana pesa hali ya kuwa anajitapa mitandaoni kuwa bilionea.

“Sasa Sam K alisema wacha leo atajui hajui, akasema mnaona yule mtu anasema ako na pesa anatoa 20k,” KRG alisema.

KRG aimlaumu Mustafa kwa kuteseka bila kusema, na kudai kuwa hawakuwa wanajua licha ya kwamba walikuwa marafiki wa karibu na muda mrefu naye.