Enock Bella asimulia jinsi alivyopata mafanikio makubwa Kenya baada ya kukataliwa TZ

Bella alisema kuwa Yamoto ilivyovunjika kila mtu alikwenda zake na yeye kila mtu alikuwa anajaribu kumfuata alikuwa anamsogeza kando, jambo lililomchochea kujaribu bahati Kenya.

Muhtasari

• Bella hata hivyo hakumlimbikizia lawama Mbosso kwa kuvunja nadhiri yake ya kwenda naye kila mahali, kwani Wasafi naye hakuwa na mamlaka ya kuingia na msanii mwenza.

Enock Bella wa Yamoto Band asimulia kwa nini alikimbia Tanzania na kuingia kenya.
Enock Bella wa Yamoto Band asimulia kwa nini alikimbia Tanzania na kuingia kenya.
Image: Instagram

Aliyekuwa msanii wa bendi ya vijana wa Yamoto, Enock Bella amesimulia jinsi alivyojipata Kenya baada ya bendi hiyo kusambaratika miaka kadhaa iliyopita na kila mmoja kwenda zake.

Katika mkutano na wanahabari, Bella alisema kuwa yeye na Mbosso ndio walikuwa watu wa mwisho kabisa kupata uongozi baada ya Aslay na Beka Flavour kupata uongozi na hata kuhama katika nyumba ambayo walikuwa wanakaa.

Baada ya kubaki peke yao, Enock na Mbosso waliweka nadhiri ya kushikana mkono popote ambapo wangeenda, lakini Mbosso alipopata nafasi ya kuingia Wasafi, Enock alibaki peke yake jambo lililomfanya kuhisi kwamba Mbosso kwa kiasi Fulani amesaliti nadhiri yao.

“Mbosso alikuwa ni sababu nyingine kunifanya pia mimi niwe Wasafi. Kwa sababu unajua, Yamoto Band wakati kila mtu aliamua kwenda kufanya harakati zake, tulibaki mimi na Mbosso. Kwa hiyo sasa ahadi ambayo tulikuwa tumewekeana mimi na Mbosso ni kwamba popote tutakapoenda, awe mimi au yeye, popote atakapoingia lazima mimi niwepo na popote nitakapoingia lazima yeye awepo. Hayo ndio yalikuwa makubaliano yetu mimi na Mbosso tu!” Bella alisema.

Lakini pia Enock hakumlaumu Mbosso kwa kushindwa kuingia na yeye Wasafi kwa kile alisema msanii huyo naye yuko chini ya uongozi na wala hana tamko lolote katika meza ya uongozi.

“Mbosso siwezi kumzungumzia vibaya kwa sababu ile menejimenti ya Wasafi oia sio yake. Yeye pia ni msanii tu. Angekuwa yeye ni mmoja wa vongozi nisingefeli. Yeye ni msanii kama mimi kwa hiyo mamlaka yake ni kwenye kufanya kazi tu.”

Kwa hiyo Mbosso alipoingia Wasafi, Enock alibaki peke yake na ikabidi aanze kupambana lakini tasnia ya muziki nchini Tanzania haikuwa inampa shavu na hivyo aliamua kufunga safari kuingia Kenya.

“Hiyo ndio sababu ilinifanya kuingia Kenya kwa ajili ya kwenda kupambana kuona sasa mbona Bongo kama ninapoingia kila mtu ananisogeza kando. Kila mtu mbona nikimfuata buana vipi ananisukuma, ngoja tutaongea,” Enock alisema.

Nchini Kenya hakukuwa kuzuri mwanzoni alipotua Mombasa lakini baadae alipata msamaria mwema akamshauri kuingia Nairobi ambapo alisema maisha yake yalipata mwamko mpya.

“Baada ya kufika Nairobi ndio ikawa nafasi yangu kubwa, nikafanya mambo mengi, mahojiano makubwa na inanipaisha hadi nikaanza kufanya video nikaona eeh sasa afadhali,” Enock alisema.