Niko tayari kusaini karatasi za talaka - Alikiba

"... kama huwezi kulimudu [jambo] basi liache. Kama huwezi kupata suluhu. Lakini kama unaweza pata suluhu, basi unafaa kutulia kabisa, unatuama kwa sababu unajua utalisuluhisha."

Muhtasari

• Msanii huyo amesema haya ikiwa ni siku tano tu baada ya mke wake Amina Khelef kukinukisha mitandaoni kwa kumtuhumu msanii huyo kwa kukataa kusaini talaka.

Alikiba avunja kimya kuhusu suala zima la talaka.
Alikiba avunja kimya kuhusu suala zima la talaka.
Image: Instagram

Msanii Alikiba amefunguka kwamba haoni tatizo katika kusaini karatasi za talaka, kama ambavyo aliyekuwa mke wake Amina Khelef alivyomtaka siku chache zilizopita.

Akizungumza baada ya kutua nchini Kenya, katika mkutano na wanahabari aliulizwa iwapo ako tayari kutekeleza wajibu wake wa kumuachia huru mke wake Khalef.

Akijibu, Alikiba japo hakujibu moja kwa moja kuwa atasaini talaka hiyo, alisema kuwa yeye ni mtu mmoja ambaye huangalia njia mbadala za kusuluhisha jambo na ikishindikana kabisa huliacha liwe insi litakavyo kuwa.

Alimaliza kwa kusema kuwa hata katika kusaini talaka hiyo si kitu kikubwa sana ambacho hawezi kukifanya, ikiwa ni mwenzake ametaka ifanyike hivyo.

“Unatakiwa kutibu msongo wa mawazo katika ile hali kwamba, kama huwezi kulimudu [jambo] basi liache. Kama huwezi kupata suluhu. Lakini kama unaweza pata suluhu, basi unafaa kutulia kabisa, unatuama kwa sababu unajua utalisuluhisha. Na hiyo ndio suluhu… kwa hiyo hata [kusaini] ile karatasi [ya talaka] sio shida. Umenielewa?” Alikiba aliuliza mwanahabari aliyemuuliza kama ameelewa alichokimaanisha kwenye maelezo yake.

Alikiba amevunja ukimya kuhusu talaka kwa mara ya kwanza, ikiwa ni siku chache tu baada ya mama watoto wake kutoka Mombasa Kenya kumkaripia vikali kupitia kurasa zake mitandaoni akisema kuwa msanii huyo amekuwa akidinda kusaini karatasi za talaka kwa kipindi kisichopungua muda wa mwaka mmoja.

Kulingana na Khelef, Alikiba kukataa kusaini talaka kunamfanya kuwa mfungwa wa ndoa asiyoitaka, na hivyo kufikiri kwamba ni muda msanii huyo angemfungua kutoka minyororo ya ndoa kwa kusaini talaka na kumweka wazi kujua kwamba yuko huru sokoni.