Alikiba: Napenda sana muziki wa Gengetone, hakuna msanii ambaye anaimba vibaya

"Hakuna msanii ambaye anaimba vibaya. Mashabiki ndio wanajua kwa sababu kila mtu ana ushabiki wake na hivyo ndio wanachagua," - Alikiba.

Muhtasari

• Msanii huyo wa ‘Utu’ alisema kuwa mjini Naivasha atatumbuiza Jumapili akiwa na bendi yake moja kwa moja jukwaani.

• Kando na Kenya, Alikiba alitaja kuzuru Rwanda na Uganda pia baadae.

Alikiba amwaga mapenzi yake kwa muziki wa Gengetone.
Alikiba amwaga mapenzi yake kwa muziki wa Gengetone.
Image: Screengrab//CitizenTV

Msanii Alikiba yuko nchini Kenya kwa ziara yake ya muziki ambapo pia anatarajiwa kutumbuiza katika hafla ya kilele cha mbio za langa langa Jumapili mjini Naivasha.

Katika mahojiano na Citizen, msanii huyo amepata kuzungumzia mapenzi yake kwa nyimbo za Gengetone ambazo zinaimbwa sana na wasanii wengi chipukizi wa Kenya, ambapo amefichua kwamba anapenda kuzisikiliza sana, haswa kipindi hiki ambapo yuko nchini.

“Mimi napenda sana Kenya, ni kama nyumbani. Huwa nasikiliza miziki ya Kenya kila wakati, kila siku. Napenda muziki wao, nausupport. Siwezi sema ni msanii mgani lakini napenda msanii ambaye anajua kuandika vizuri. Gengetone napenda, naisikiliza sana. Mara nyingi unajua nikiwa Kenya, nitasikiliza muziki gani? Nawajua wasanii wa Kenya, namjua ni yupi master….” Alisema.

 “Mimi naamini wasanii wote wana vipaji, wanatia bidii na wanafnaya kazi nzuri. Hakuna msanii ambaye anaimba vibaya. Mashabiki ndio wanajua kwa sababu kila mtu ana ushabiki wake na hivyo ndio wanachagua sio mimi,” Alikiba aliongeza.

Msanii huyo wa ‘Utu’ alisema kuwa mjini Naivasha atatumbuiza Jumapili akiwa na bendi yake moja kwa moja jukwaani na kuwataka watu wote kujitokeza kwa wingi kujipakulia raha ya tamasha lake.

Alikiba pia katika rundo la nyimbo zake nyingi Zaidi ya miongo miwili, alisema kuwa anaipenda sana ngoma ya ‘Utu’ ambayo akiingia tu kwenye jukwaa hivi anafunika kila kitu.