Ezekiel Mutua awashutumu wasanii wa nyimbo za injili

"Nafikiria Erick Omondi alikuwa sawa akisema kuwa kuna kitu ambacho hakiko sawa na wasanii wa nyimbo za injili" alisema Mutua.

Muhtasari

• Ezekiel amesema kuwa wasanii wa nyimbo za injili wamemsababishia uchungu mkubwa katika juhudi zake za kufufua sekta ya muziki nchini Kenya.

• Kulingana na Ezekiel, tasnia hii ina waigizaji wengi na wasanii halisi wa injili ni wachache.

Mkurugenzi mkuu wa chama cha hakimiliki za muziki Kenya, MCSK Ezekiel Mutua
Mkurugenzi mkuu wa chama cha hakimiliki za muziki Kenya, MCSK Ezekiel Mutua
Image: Facebook//EzekielMutua

Afisa mkuu mtendaji wa baraza la hakimiliki za muziki Kenya (MCK), Ezekiel Mutua amemuunga mkono mchekeshaji Erick Omondi kuwakejeli wasanii wa nyimbo za injili.

Ezekiel amesema kuwa wasanii wa nyimbo za Injili wamemsababishia uchungu mkubwa katika juhudi zake za kufufua sekta ya muziki nchini Kenya.

"Tangu nijiunge na MCK mwaka mmoja uliopita, watu ambao wamenipa maumivu zaidi katika juhudi zangu za kufufua sekta ya muziki nchini ni wasanii wa nyimbo za injili."

Katika taarifa aliyochapisha katika ukurasa wake wa Facebook, Ezekiel alikiri kuwa katika muda wa mwaka mmoja akihudumu kama afisa mkuu mtendaji wa MCK ameweza kuthibitisha madai yaliyotolewa na mchekeshaji Erick Omondi.

"Nafikiria Erick Omondi alikuwa sawa akisema kuwa kuna kitu ambacho hakiko sawa na wasanii wa nyimbo za injili"

Kulingana naye tasnia hii ina waigizaji wengi na wasanii halisi wa injili ni wachache.

Mwaka jana Erick Omondi aliwashambulia vikali wasanii wa nyimbo hizo kwa kile ambacho alisema ni kuzembea kazini, na hata aliwalaumu wasanii hawa kuacha kufanya nyimbo za injili na kuingililia muziki wa kidunia.

Malalamishi haya yanajiri siku mbili tu baada ya msanii maarufu kutoka Kisii, Christopher Musyoma almaarufu Embarambamba, kuchapisha video iliyozua mdahalo mkubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuonekana amevalia mavazi ya kike.

Video hiyo iliweza kuibua hisia kinzani kutoka kwa wafuasi wake ambao walihisi kuwa msanii wa nyimbo za injili hapaswi kufanya mambo ambayo hayakubaliani na kitabu kitakatifu, bibilia.

Embarambamba alijitokeza na kujitetea vikali na kusema kuwa hii ilikuwa mojawapo ya njia ya wasanii kutafuta hela katika taaluma yao ya muziki na kuweza kuongeza umaarufu.

"Hapa ndio tumefika kama wasanii, unajua lazima tutafute vile tutakula na vile tunasambaza jina."