Mtangazaji Gidi asherehekea miaka 7 tangu kupata Shahada ya Uzamili

Gidi alifanya KCSE katika shule ya upili ya Aquinas kisha kuendeleza masomo yake katika vyuo vikuu vya JKUAT , KCA na Strathmore.

Muhtasari

•Mtangazaji huyo tajika alifufua kumbukumbu ya tarehe 24 Juni, 2016  ambapo alitawazwa kwa Shahada yake ya kwanza ya Uzamili.

•Hivi majuzi alihitimu kama Mwanasayansi wa Takwimu aliyeidhinishwa kuongeza juu ya sifa zake kubwa za masomo.

Gidi amesherehekea miaka 7 tangu kupata Shahada ya Uzamili
Image: FACEBOOK// JOE GIDI

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi Ogidi ameadhimisha miaka saba tangu alipohitimu na Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara kutoka Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Strathmore.

Siku ya Jumamosi, Juni 24, mtangazaji huyo tajika alifufua kumbukumbu ya tarehe 24 Juni, 2016  ambapo alitawazwa kwa Shahada yake ya kwanza ya Uzamili.

"Tayari ni miaka 7," Gidi aliandika chini ya chapisho hilo la kumbukumbu.

Katika chapisho hilo la miaka saba iliyopita, mwanamuziki huyo wa zamani alishiriki picha zake kadhaa akiwa pamoja na baadhi ya wanafunzi wenzake wa zamani ambazo zilipigwa mnamo siku ya kuhitimu.

Hii ilikuwa baada ya kuhitimu shahada ya uzamili kutoka chuo kikuu hicho chenye makao yake makuu jijini Nairobi.

Gidi alifanya mtihani wake wa KCSE katika Shule ya Upili ya St Thomas Aquinas jijini Nairobi mwaka wa 1999 kabla ya kujiunga na chuo kikuu cha KCA na cha JKUAT ambapo alihitimu na shahada ya Habari na Teknolojia.

Hivi majuzi alihitimu kama Mwanasayansi wa Takwimu aliyeidhinishwa kuongeza juu ya sifa zake kubwa za masomo.

Gidi alihitimu na kupokea cheti chake kutoka Chuo Kikuu cha Texas katika jimbo la Austin, Marekani baada ya kumaliza masomo yake ya Uzamili katika Sayansi ya Data na Uchambuzi wa Biashara katika Shule ya Biashara ya McCombs.

Huku akisherehekea ushindi huyo, mwimbaji huyo wa zamani alitoa shukrani za dhati kwa chuo hicho cha Marekani kwa mafunzo aliyopokea.

"Mwanasayansi wa Data aliyeidhinishwa, asante Chuo Kikuu cha Texas, Shule ya Biashara ya McCombs kwa mafunzo ya kina," alisema.

Mtangazaji huyo aliambatanisha ujumbe wake na picha ya cheti ambacho alikabidhiwa baada ya kukamilisha masomo yake.

Cheti hicho kilionyesha kuwa alihitimu mwezi uliopita, Machi.

Mtangazaji mwenzake, Jacob 'Ghost' Mulee alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kumpongeza kwa ushindi huo.

"Hongera bosi," alisema.

Miezi uliopita, mtangazaji huyo alianza jaribio lake la nne la kujifunza lugha ya Kifaransa baada ya kushindwa katika majaribio yake matatu ya awali.