Kwa Biblia napenda Judas Iscariot kuliko Petro - Gaucho

“Ndio maana wakati Yesu alichukuliwa kwenda kufa, Judas aligundua kumbe amekosa. Haikuwa makosa yake, yeye alikuwa ameamini kwamba Yesu hawezi kuuawa.” - Gaucho.

Muhtasari

• “Petro alikataa Yesu. Aliulizwa unajua huyu mtu, akasema hapana mimi huyu mtu hata msinihusishe na yeye." - Gaucho.

Gaucho aeleza sababu ya kumpenda Judas kuliko Petro kwenye Biblia.
Gaucho aeleza sababu ya kumpenda Judas kuliko Petro kwenye Biblia.
Image: Facebook

Gaucho, rais wa bunge la wananchi amefichua kwamba katika maisha yake alipofika Nairobi aliwahi pata ufadhili wa kwenda katika shule ya mafunzo ya Biblia kusomea uhubiri.

Mwanaharakati huyo alikuwa akizungumza na Oga Obinna ambapo alipata kusimulia jinsi alijipata Nairobi baada ya wazazi wake kufa, akajiunga na timu za mitaani kucheza mpira na baadae akajipata katika shule ya mafunzo ya Biblia.

Baada ya kuhitimu, alirudi mitaani kuzungumza na vijana wanaojihusisha katika ujambazi.

Gaucho katika mahojiano hayo alifunguka kuwa yeye katika mafunzo ya Biblia anaenda kinyume na wengi sana baada ya kukiri kwamba anampenda mhusika mmoja ambaye alikuwa mwanafunzi wa Yesu – Judas Iscariot.

Kwa wale wamebukua Biblia sana wanaamini kwamba Judas si mtu anayepaswa kutumiwa kama mfano chanya kaitka jamii kwa kuamini kwamba ni yeye alimsaliti Yesu kwa wanajeshi wa Pilato.

Lakini kwa Gaucho, Judas Iscarioti ni mzuri kuliko Petro ambaye alikuja kumkana Yesu dakika za mwisho.

“Katika Biblia, Mimi nampenda Judas kuliko Petro. Judas hakupenda kusaliti Yesu. Judas aliamini Yesu sana kwa sababu wakati hao watu walimpelekea maneno ya kwamba tunataka Yesu tunataka kumshika, Judas aliangalia hawa watu akaona ni kama wanafanya mzaha. Yesu ambaye amefufua Lazaro, ametembea juu ya maji…. Ule ujasiri ambao Judas alikuwa nao kwa Yesu akijua kwamba Yesu hawezi kufa, ndio maana alichukua ile pesa akicheka na kusema nyinyi wacha tu nikule hizi pesa za bure kwa sababu huyu jamaa vile mimi najua hamwezi muua,” Gaucho alielezea sababu yake kumkubali Petro.

“Ndio maana wakati Yesu alichukuliwa kwenda kufa aligundua kumbe amekosa. Haikuwa makosa yake, yeye alikuwa ameamini kwamba Yesu hawezi kuuawa.”

Kwa upande mwingine, alikuwa na sababu ya kutomkubali Petro licha ya wengi kumfagilia kama mmoja ambaye alisimama na Yesu na hata baada ya kifo chake kuendeleza injili aliyoacha Yesu.

“Petro alikataa Yesu. Aliulizwa unajua huyu mtu, akasema hapana mimi huyu mtu hata msinihusishe na yeye. Thomas alisema kuwa ili aamini kumfuata Yesu sharti angeonesha alama za misumari. Kwa hiyo kati ya Judas, Petro na Thomas, nani alikuwa anamjali Yesu?” Gaucho aliuliza.

Alisema kuwa katika siasa, kuna watu wengi ambao wako nyuma ya Raila Odinga lakini ambao hawataki awe rais, akiwafananisha na Thomas na Petro.