Ezekiel Mutua azidi kuwainjika Ssaru na Fathermoh kwenye tanuru la moto bila huruma

"Watu wengi wasingependa watoto wao wasikilize upuuzi wenu kuhusu uasherati na kujamiiana. Ati "niko na pesa na ni ya babako." Kweli? - Mutua alisema.

Muhtasari

• "Kwa kweli mashirika mengi hayahusishi chapa zao na uchafu kwa hivyo unajitenga na pesa nyingi huku ukifurahisha watu wasiowajua" - Mutua.

Ezekiel Mutua aendeleza vita dhidi ya Sasaru na Fathermoh
Ezekiel Mutua aendeleza vita dhidi ya Sasaru na Fathermoh
Image: Screengrab (YouTube), Facebook.

Mkurugenzi mtendaji wa MCSK Dkt Ezekiel Mutua ameendeleza mashambulizi na chukizo lake dhidi ya watunzi wa wimbo wa Gengetone, ‘Kasikie vibaya huko kwenu’ akisema kuwa vijana hao Ssaru na Fathermoh hawajafanya vizuri kupuuzilia mbali kile alichokiita ushauri wa watu wazima.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mutua alichapisha aya ndefu akiteta kwamba wasanii hao hawafai hata kuwa na fahari kwa mafanikio makubwa ya ngoma hiyo, kwani maudhui yake kiujumla ni ya kupotosha na ambayo hayapaswi kupigiwa saluti na watu.

Mutua alisema kuwa kwa kuendelea kutoa nyimbo zenye maudhui machafu, wasanii wanawafurahisha watu wasiowajua mitandaoni na kupewa tu ahasante ya mdomo huku wakiendelea kujitenga mbali na makampuni ya kibiashara ambayo yangewapa mkataba wa hela nono kama mabalozi wao, kwani makampuni mengi hayawezi kujihusisha na watu wenye maudhui chafu.

“Kwahiyo unafanya wimbo mmoja mchafu na inakufika kichwani hadi ukatupilia mbali ushauri wa wazee na wataalamu waliobobea kwa kuwafukuza kwa kuwapungia mkono "Kaskie Vibaya na huko kwenu?" Mutua aliuliza.

“Halafu wageni wanapandisha matusi na majivuno yako kwenye mitandao ya kijamii na kujiona uko juu ya dunia. Ni wimbo uliovuma katika vilabu vyote vya usiku. Lakini vituo na vilabu vya usiku vinavyotumia wimbo wako havikulipi chochote, au kama kuna chochote, karanga. Kwa kweli mashirika mengi hayahusishi chapa zao na uchafu kwa hivyo unajitenga na pesa nyingi huku ukifurahisha watu wasiowajua kwenye mitandao ya kijamii,” Mutua aliongeza.

Mutua alisema kuwa wasanii hao baada ya kupata umaarufu kutokana na maudhui chafu yasiyowalipa, wanamalizia kuwa fukara. Wasanii hao huogopa hata kuomba msaada kwa sababu walichoma picha na kuishia kujuta katika hali ya kutamauka na msongo wa mawazo kimya kimya.

“Kwa hivyo wacha nizungumze nawe leo kama baba. Kupuuza ushauri kutoka kwa watu wanaokupenda kweli na wanaotaka mema kutoka kwako ni mwanzo wa mwisho. Watu wengi wasingependa watoto wao wasikilize upuuzi wenu kuhusu uasherati na kujamiiana. Ati "niko na pesa na ni ya babako." Kweli? Ikiwa hiyo ingekuwa hadithi ya kweli, mhusika hangejivunia,” Mutua alisema.