Gaucho alazwa hospitalini baada ya kushambuliwa kwa silaha kali Kamukunji

"Namshukuru Mungu nilifanikiwa kutoroka baada ya kupata majeraha mabaya. Kwa sasa niko hospitali nikipokea matibabu,” Gaucho aliandika

Muhtasari

• Haijulikani waliomshambulia ni kina nani na nia yao ilikuwa gani, lakini wafuasi wake walifurika kwenye chapisho hilo wakimtakia afueni ya haraka.

Gaucho alazwa baada ya kushambuliwa.
Gaucho alazwa baada ya kushambuliwa.
Image: Facebook

Calvince Gaucho, ambaye ni kiongozi wa bunge la wananchi amelazwa hospitalini baada ya kudai kushambuliwa na kundi la watu ambao hawajui siku ya Jumanne akielekea katika uwanja wa Kamukunji.

Gaucho ambaye ni mtetezi na mkereketwa mkuu wa sera za kiongozi wa Azimio Raila Odinga alipakia picha akiwa amelazwa katika kitanda cha hospitalini na kusema kuwa alishambuliwa katika uwanja wa Kamukunji.

“Jana nilivamiwa na kundi la watu wasiojulikana wakiwa na silaha wakati nikielekea kwenye mkutano wa Kamkunji lakini namshukuru Mungu nilifanikiwa kutoroka baada ya kupata majeraha mabaya. Kwa sasa niko hospitali nikipokea matibabu,” Gaucho aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Taarifa za kushambuliwa kwake kunakuja siku chache baada ya kuibuka mgawanyiko katika mrengo wa Azimio kuhusu kijana huyo ambapo wengine wamekuwa wakimtuhumu kuwa anakwenda kinyume na sera za Odinga.

 Hata hivyo, katika mahojiano na Obinna, Gaucho aliweka wazi kwamba yeye ni mwanachama wa kudumu wa chama cha ODM na kuweka wazi kwamba ana heshima kubwa sana kwa kiongozi huyo mkongwe wa mrengo wa siasa za upinzani nchini Kenya.

Haijulikani waliomshambulia ni kina nani na nia yao ilikuwa gani, lakini wafuasi wake walifurika kwenye chapisho hilo wakimtakia afueni ya haraka.