Diamond ageuka mbogo, "Mmewapa vichwa wasanii wasio level yangu kushindana nami!"

"Wakati naanza harakati za kutoka nje ya EA wengi mlichelewa kunielewa na mkaanza kusema ‘ooh nimeishiwa utunzi, ooh naimba ujinga’ na kashfa kibao. Sitaki maoni wala ushauri na ushuzi..”

Muhtasari

• Hata hivyo msanii huyo wa WCB Wasafi alisema kuwa kupitia yeye, wengi wamefahamu kumbi maarufu duniani ambazo ametumbuiza.

• Kwa maneno ya Diamond, Watanzania walikuwa wanazisoma kumbi hizo kwenye ramani za jeografia kabla ya yeye kufika kule.

Diamond aonesha kuchukizwa na kulinganishwa na wasanii duni.
Diamond aonesha kuchukizwa na kulinganishwa na wasanii duni.
Image: Facebook

Diamond Platnumz, Simba wa muziki wa kizazi kipya Afrika Mashariki ameibuka na hasira za mkizi kuhusu kusemwa na kusimangwa kwamba ameishiwa na ubunifu wa kuandika miziki mizuri.

Kupitia Instastory yake, Diamond aliachia cheche kali kwa watu wanaojaribu kumkemea kwa ukimya wake wa miezi kadhaa bila kutoa muziki huku akisema kuwa atarejea kwa kishindo cha mngurumo wa tembo.

Diamond aliwasuta mashabiki hao akisema kuwa kwa muda ambao amekuwa kimya, amepata maneno baadhi wakimshindanisha na wasanii wa viwango na hadhi zisizooana na za kwake, na kwamba kuanzia mwezi Julai anakuja kuwanyamazisha kwa kile alikitaja kuwa ni ‘mvua ya mawe’.

“Kwa mwezi Julai, itaanza rasmi mvua ya mawe… zangu collabo za nje na za ndani. Na nitahudumu hapo kwa No.1 on trends kuanzia Julai 2023 hadi Januari 2024. Wakati naanza harakati za kutoka nje ya EA wengi mlichelewa kunielewa na mkaanza kusema ‘ooh nimeishiwa utunzi, ooh naimba ujinga’ na kashfa kibao. Mkaanza kuwapa vichwa wasanii wasio level yangu kushindana na mimi…” Diamond alifoka.

Hata hivyo msanii huyo wa WCB Wasafi alisema kuwa kupitia yeye, wengi wamefahamu kumbi maarufu duniani ambazo ametumbuiza, na ambazo kabla yake wengi walikuwa wanaishia kuzisoma kwenye ramani za jeografia tu.

Alisema kuwa alibeba jina la Bongo Flava kwenye mabega yake mwenyewe kwenda rubaa za kimataifa wakati wasanii hao alioanza kushindanishwa nao walikuwa wanasubiria shoo za kuandaliwa na vituo vya Redio nchini mwao.

Diamond aliwataka wakosoaji wake kukoma kumpa ushauri, akisema kuwa yuko tayari kuwalipuakwa mashambulizi yake pasi ya wao kujibu na kuwataka ushauri wao wajiwekee.

“Hivyo kama mlivyokaa kwa kutulia wakati natega mabomu yangu ya kutoka nje ya EA naomba pia make kwa kutlia vivyo hivyo ninapoanza mashambulizi yangu. Sitaki maoni wala ushauri na ushuzi..” Diamond aliwaga radhi bayana.