UCHUMI KENYA

Eric Omondi kuendelea na 'tour' ya michango kwa ajili ya Wakenya walala hoi

Nimekusanya karibu Ksh140,000 za kuwasaidia Wakenya wenzangu kununua unga - Eric Omondi

Muhtasari

•Katika shughuli yake ya kuomba pesa, mwenyewe Omondi aliongoza kwa wimbo wa kutoa sadaka huku akieleza hali ya uchumi nchini Kenya.

• Toa ndugu toa dada, ulicho nacho, Mungu anakuona mpaka moyoni mwako...uchumi ni mbaya Kenya.

Eric Omondi akiwa Ddoma, Tanzania akiomba pesa za kuwasaidia Wakenya kununua unga
Eric Omondi akiwa Ddoma, Tanzania akiomba pesa za kuwasaidia Wakenya kununua unga
Image: Eric Omondi// INSTAGRAM

Mkuza maudhui nchini Kenya Eric Omondi amedakia kuwa kwa sababu ya hali ngumu ya kimaisha inayoendelea kushuhudiwa humu nchini, atatembea popote ulimwenguni ili aweze kuomba msaada wa fedha za kuwasaidia Wakenya wenzake.

Msanii huyo ameeleza hayo alipokuwa katika mji wa Dodoma nchini Tanzania, alipokuwa akichangisha pesa kwenye hafla fulani maabadini ambapo alikiri kuwa alichangisha zaidi ya Ksh140,000.

Kenya nimesikia petroli imepanda. Mimi jana pale Dodoma niliendelea kuchanga hela za kuwasaidia Wakenya wenzangu. Nilikusanya karibu Ksh140,000. Nimeanza rasmi mpango wa “WOIYEE TOUR” Nitakuwa nikitembea ulimwenguni kote nikiomba pesa katika kila mji,” alisema Eric Omondi.

Haya yanajiri punde tu, sheria ya mwaka wa fedha 2023 inayohusu kuongezeka kwa ushuru ilipoanza kufanyishwa kazi kuanzia Julai 1, ambapo mkuza maudhui huyo aliamua kuzuru taifa jirani la Tanzania huku akiwa amevalia viatu vilivyobwerebweta.

Katika shughuli yake ya kuomba pesa, mwenyewe Omondi aliongoza kwa wimbo wa kutoa sadaka huku akieleza hali ya uchumi nchini Kenya.“ Toa ndugu toa dada, ulicho nacho, Mungu anakuona mpaka moyoni mwako...uchumi ni mbaya Kenya,” aliendelea.

Mwezi mmoja uliopita, msanii huyo alikuwa London, Uingereza kwa shughuli hiyo hiyo ya kuomba pesa za kuwasaidia Wakenya kununua unga pamoja na wakuza maudhui wenzake kununua vipakatalishi, ambapo alikiri kuwa alikusanya zaidi ya laki tatu pesa za Kenya.

Baadhi ya wanamitandao wameweza kutoa hisia zao kwake, kuhusu tabia ya kuomba pesa, ambapo baadhi wanasema kuwa anaibisha serikali huku wengine wakidai serikali iabishwe hadi iwajali raia wake.“ Sasa hii imekuwa nyingi sana! Nani alikuruhusu kutembea kuomba pesa ukitumia jina la Wakenya?” Mmoja wa wanamitandao aliuliza.

Vile inafaa...aibisha hii serikali kabisa hadi kieleweke!” Mwingine alidakia.