Diamond, Alikiba na Harmonize kufanya collabo ya pamoja ya wimbo wa klabu ya Yanga

"Wote! Huyu anaweza akaanza Yoh... huyu mwingine akaanza [kukohoa].. yaani tunawachanganya wote,”

Muhtasari

• Baadhi walihisi kwamba hizi ni porojo tu lakini wengine pia wakasema kuwa hakuna linaloshindikana na wasanii hao bila shaka watazika tofauti zao ‘Siku ya Wananchi’.

• Diamond na Alikiba kwa muda mrefu wamekuwa wasanii wasioweza kuonana huku kila mmoja akikwepa kabisa kuzungumzia mwenzake pindi anapobanwa na maswali.

Alikiba, Diamond, Alikiba kukutana kwenye jukwaa moja.
Alikiba, Diamond, Alikiba kukutana kwenye jukwaa moja.
Image: Instagram

Mwaka huu katika wiki ya Wananchi, ambayo ni wiki inayoandaliwa kusherehekea timu ya Yanga nchini Tanzania, taarifa za ndani mwa klabu hiyo zinasema kwamba wanapanga kuwaunganisha pamoja kwa mara ya kwanza wasanii wanaoishabikia timu hiyo na ambao ni mahasidi kivyao.

Katika video moja ambayo imekuwa ikienezwa, ilimuonesha afisa wa habari wa timu hiyo Ali Kamwe akitoa mipango kuhusu wiki hiyo ambayo itaandaliwa mwezi kesho.

Ali Kamwe alisema kuwa watafanikisha kuwaleta pamoja Diamond Platnumz ambaye walifanikiwa kumnyakua kutoka kushabikia Simba mwezi jana, pamoja na mashabiki wa muda mrefu wa Yanga Alikiba lakini pia Harmonize na wote watatu watafanya collabo ya wimbo wa Yanga.

“Tutapata burudani ya wasanii bora kabisa barani Afrika kwenye wiki ya wananchi. Sasa wakiuliza, kwa hiyo mtawaunganisha wote kwenye jukwaa moja? Ndio! Wote amabo mnawajua ni wasanii wa Yanga watapanda kwenye jukwaa moja kwa heshima ya Klabu yetu. Na watawapa burudani siku hiyo,” Ali Kamwe alisema.

“Kama kuna mtu alikuwa kwenye lebo Fulani akatoka, atakutana na bosi wake siku hiyo. Na wataimba. Hivo tunafanya mpango waimbe wimbo wa Yanga wote. Eeh piga chorus, verse namba moja namba mbili, piga kibwagizo … wote! Huyu anaweza akaanza Yoh... huyu mwingine akaanza [kukohoa].. yaani tunawachanganya wote,” Ali Kamwe aliongeza.

Baadhi walihisi kwamba hizi ni porojo tu lakini wengine pia wakasema kuwa hakuna linaloshindikana na wasanii hao bila shaka watazika tofauti zao ‘Siku ya Wananchi’.

Diamond na Alikiba kwa muda mrefu wamekuwa wasanii wasioweza kuonana huku kila mmoja akikwepa kabisa kuzungumzia mwenzake pindi anapobanwa na maswali.

Harmonize alijiunga kwenye orodha ya mahasidi wa Diamond miaka ichache iliyopita baada ya kupishana maelewano na kuondoka WCB Wasafi kwa kishari mno.