Diamond amuamrisha Lavalava kukaa pembeni na kumuacha atawale chati za muziki

Diamond alitoa tamko hili wiki moja ikiwa ndio Lavalava amekuwa akitrend na wimbo wake mmoja, huku yeye akiwa ndio amerejea kwafujo akiahidi mvua ya mawe kuanzia Julai hadi Januari mwakani.

Muhtasari

• "Si tumekubaliana wenyewe kwa wenyewe Wasafi na tunaoheshimiana nao… mbona tena tunafanyiana hiyana wenyewe kwa wenyewe tajiri,” Diamond alimwambia Lavalava.

Diamond amkumbuka Lavalava baada ya muda mrefu wa kumpotezea
Diamond amkumbuka Lavalava baada ya muda mrefu wa kumpotezea
Image: Facebook

Msanii nguli wa Bongo Flava, Diamond Platnumz amemtaka msanii wake Lavalava kukaa pembeni kidogo kimuziki na kumuachia uwanja kutamba na ujio wa ngoma zake mpya ambazo alizitaja kama ujio wa mvua ya mawe.

Diamond aliandika haya baada ya kugundua kwamba Lavalava ndiye msanii anayezidi kutamba kwenye jukwaa la YouTube kwa nchini Tanzania, na hivyo kumtaka kupunguza kasi yake kidogo ili kumpisha naye atambe kiasi – saa chache tu baada ya kuachia kibao chake kipya ‘My Baby’ akimshirikisha msanii wa Nigeria, Chike.

Kwa mujibu wa picha ya skrini ambayo Diamond alipakia kwenye Insta story yake, msanii Lavalava ndiye gumzo kubwa kwenye jukwaa la YouTube nchini Tanzania, shukrani kwa kibao chake kipya cha ‘Tajiri’ ambacho kimempa uhai tena baada ya kupotea kwa Zaidi ya miaka miwili bila kusikika.

Wimbo wa Diamond wa My Baby ulikuwa unafuata katika nafasi ya pili, na hivyo kumfanya msanii huyo kutoa kile kilichoonekana kama ombi kwa Lavalava kumpisha kidogo ili naye ashikilie usukani katika jukwaa hilo la video.

“Lavalava, hebu niache basi na mie nikae hapo namba moja… si tumekubaliana wenyewe kwa wenyewe Wasafi na tunaoheshimiana nao… mbona tena tunafanyiana hiyana wenyewe kwa wenyewe tajiri,” Diamond aliandika.

Msanii huyo alinukuu maneno yake ambayo alisema siku chache zilizopita wakati anawakoromea baadhi ya wadau katika muziki ambao walikuwa wanamsuta kuwa amepoa sana kama mtu ambaye amekosa maarifa na ubunifu wa kutunga mashairi mapya.

Msanii huyo aliahidi kurejea Julai hadi Januari mwakani, akisema kuwa atashikilia namba moja kwenye chati za muziki na hatowapa nafasi wasanii wengine isipokuwa wasanii wa Wasafi tu na wahache wa nje ambao wanaheshimiana nao.