Kichwa cha habari 'Nzi afia kidondani' kueleza kifo cha padri chamkera Ezekiel Mutua

"Huwezi kumdhihaki mtu aliyekufa kwa njia hiyo bila kujali mazingira yanayozunguka kifo chake" - Mutua alisema kwa kukerwa.

Muhtasari

• Alitoa wito kwa baraza la wanahabari nchini MCK kuingilia kati na kuhakikisha ubora katika kuunda vichwa vya habari humu nchini kwa kujali pande zote.

Ezekiel Mutua akubaliana na kauli ya mchungaji Tony Kiamah kuwa wachungaji hawafai kuitwa wazazi kwa waumini.
Ezekiel Mutua akubaliana na kauli ya mchungaji Tony Kiamah kuwa wachungaji hawafai kuitwa wazazi kwa waumini.
Image: Facebook

Mkurugenzi mkuu wa MCSK Ezekiel Mutua ameonyesha kero lake dhidi ya runinga moja ya humu nchini ambayo ilitumia kichwa cha habari cha dhihaka kuelezea kifo cha padre mmoja nchini muda Fulani nyuma.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mutua alisema kuwa runinga moja ya humu nchini ilitumia kichwa cha habari alichokitaja kama cha dhihaka ambacho kilikuwa ‘Nzi afia kidondani’ kujaribu kuelezea muktadha wa padre wa kanisa katoliki aliyefariki katika kaunti ya Nyeri.

“Moja ya vichwa vya habari vya kuudhi na kusikitisha ambavyo nimewahi kuviona kwenye habari ni "Nzi afia kidondani" kwenye moja ya vituo vya televisheni vilivyoongoza saa moja kamili usiku. Ilikuwa ikirejelea kifo cha kasisi wa Kikatoliki huko Nyeri,” Mutua alisema.

Mkurungenzi huyo wa MCSK alisuta kituo hicho cha runinga akisema kuwa haikufaa kabisa kutumia kichwa cha habari kinacholenga kudhihaki kifo cha mtu, kwani hiyo ni sawa sawa na kumkosea marehemu heshima.

“Hii haina moyo, haina hisia na haina taaluma kwa kiwango kingine. Huwezi kumdhihaki mtu aliyekufa kwa njia hiyo bila kujali mazingira yanayozunguka kifo chake. Isingekuwa bora kama angekufa katika ajali. Yeye ni binadamu, anastahili heshima,” Mutua alionesha kukerwa.

Mutua alisuta mhariri wa kichwa hicho cha habari akisema kuwa kujishusha kwa kiwango hicho ili kujaribu kuunda kichwa cha habari cha kuwafurahisha watu ni akili ya mtu mgonjwa, kwani mtu unayejaribu kumdhihaki ana ndugu, jamaa na familia ambao unawaumiza kihisia.

“Ana jamaa na marafiki wanaomlilia. Kujishusha chini kwa jina la kuunda kichwa cha habari ni kazi ya akili mgonjwa,” alisema.

Alitoa wito kwa baraza la wanahabari nchini MCK kuingilia kati na kuhakikisha ubora katika kuunda vichwa vya habari humu nchini kwa kujali pande zote.

“Hili ni jambo ambalo Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya linafaa kuchukua hatua mara moja. Vyombo vya habari vinapaswa kuomba radhi na wanahabari wetu lazima wafunzwe kuwa wasikivu wanaporipoti visa kama hivyo,” alisema.

Matamshi ya Mutua yanakuja siku moja tu baada ya habari sawia za kifo cha padre katika mgahawa mmoja nchini Murang’a akiwa na kidosho kuvuma kote mitandaoni na kwenye vyombo vya habari.