Jalang'o ajuta kuacha utangazaji na kuwa MP," Utangazaji una pesa kuliko Ubunge!"

"Watu wanasema ni karibu milioni moja na ikitozwa ushuru inakuja kama laki nane. Hiyo ni kama nusu na kile nilikuwa nalipwa kama mtangazaji," - Jalang'o.

Muhtasari

• "Ukiwa kwenye ulingo wa siasa wananchi ni wale wale." - Jalang'o.

• "Kwa mwanasiasa wananchi wanakuona kama suluhisho, kwa mwanahabari wananchi wanakuona kama utakayetoa maono yao ili mheshimiwa sasa aweze kuyatatua,” - Jalang'o.

Mbunge wa Lang'ata ajita kuingia kwenye siasa.
Jalang'o Mbunge wa Lang'ata ajita kuingia kwenye siasa.
Image: Facebook

Mbunge wa Lang’ata ambaye alikuwa mchekeshaji na mtangazaji wa redo, Jalang’o amejuta kuacha utangazaji katika kituo cha redio na kuhamia siasa.

Jalang’o alifichua haya wakati aliketishwa kwenye kigoda cha runinga ya NTV na mwanahabari Fredrick Muitiriri.

Alisema kwamba watu wengi wana kasumba ya kuona kuwa kuingia katika siasa ni njia ya haraka ya mtu kutajirika, na kusema kuwa akiwa mtangazaji alikuwa anapata mshahara mnono kuliko hata ule ambao anapata kama mbunge.

“Ukitaka kuingia siasa kutengeneza pesa, utaumia sana. Siasa haitaki mtu ambaye anakuja na tamaa ya kusema kuwa nataka kuwa mbunge ili nipate utajiri. Mimi nikiwa mwanahabari naeza kuambia nilikuwa nalipwa Zaidi kuliko ninavyolipwa sasa hivi. Ha hiyo ilikuwa ni pesa yangu mwenyewe,” Jalang’o alisema.

Mbunge huyo mtata alisema kuwa sasa hivi mshahara anaolipwa hawezi kuupangia mambo yake ya kibinafsi kwani kuna mambo mengi ambayo yanamhitaji na kulazimu kuingia mfukoni mwake.

“Sasa hivi nikilipwa, kuna matanga mahali, mgonjwa, karo ya shule. Tena inataka utu kabisa. Watu wanasema ni karibu milioni moja na ikitozwa ushuru inakuja kama laki nane. Hiyo ni kama nusu na kile nilikuwa nalipwa kama mtangazaji,” Jalang’o aliweka wazi sikitiko lake.

Mbunge huyo pia alipata kugusia kwa kiduchu tofauti iliyopo kati ya siasa na uanahabari.

“Tofauti ni kubwa sana, isipokuwa kama naweza ona zote ni Sanaa tu. Maanake katika uanahabari bado unashughulikia wananchi na hata hapa tulipo ni wananchi tunataka kuwashughjulikia. Ukiwa kwenye ulingo wa siasa wananchi ni wale wale. Kwa mwanasiasa wananchi wanakuona kama suluhisho, kwa mwanahabari wananchi wanakuona kama utakayetoa maono yao ili mheshimiwa sasa aweze kuyatatua,” Jalang’o alisema.