Mbunge Jalang'o: Watu wengi wameniita 'one term MP' na ninashukuru

“Hii ni nafasi ambayo ametupa mwenyezi Mungu. Na ni wananchi ndio wametupa kazi. Wananchi weneywe wakisema huwezi kufanya kazi tena, ni hivyo" - Jalang'o.

Muhtasari

• Jalang’o alisema kuwa huwa anakutana na wana Lang’ata nyanjani na anawaambia bila kubeta kwamba ameamua kufanya na rais kazi.

Jalang'o azungumzia kuitwa mbunge wa mhula mmoja.
Jalang'o azungumzia kuitwa mbunge wa mhula mmoja.
Image: Facebook

Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o hatimaye amezungumzia suala la wengi ambao hawapendi sera zake za kisiasa kushirikiana na upande wa serikali licha ya kuwa mbunge wa upinzani kutoka ODM.

Katika mahojiano ya kipekee usiku wa Jumatatu kwenye runinga ya NTV, Jalang’o alifunguka hisia zake pindi anaposikia na kuona mitandaoni wengi wakimuita mbunge wa muhula mmoja na kusema kwamba hana tatizo na hilo, kwani azma yake kubwa ni kuwafanyia wana Lang’ata kazi katika kipindi hiki cha miaka mitano ambacho ameteuliwa.

Jalang’o alisema kuwa haogopi kuwa mbunge wa muhula mmoja alipoulizwa iwapo naye anaona akifuata mkondo ambao umekuwa ukishuhudiwa katika eneobunge hilo tangu mwaka 2013 ambapo kila mbunge amekuwa akimaliza muhula mmoja tu na kutemwa nje na wananchi.

“Hii ni nafasi ambayo ametupa mwenyezi Mungu. Na ni wananchi ndio wametupa kazi. Wananchi weneywe wakisema huwezi kufanya kazi tena, ni hivyo. Nimeitwa kufanya kazi kwa Lang’ata kwa miaka mitano. Wao tu ndio wataamua kama watanipa nafasi nyingine tena,” Jalang’o alisema.

“Wengi wameniita one-term MP, na mimi nazidi kuwaambia hata huo muhula mmoja tu nashukuru Mungu kwa sababu hakuna katika ndoto zangu, zote kutoka nilipozaliwa, maisha ambayo nimepitia kudhani kwamba leo ningekuwa Mbunge wa Lang’ata. Sikuwahi fikiria. Huo muhula mmoja tu….” Jalang’o aliongeza.

Mchekeshaji huyo wa zamani alisisitiza kwamba ni Mungu amempa nafasi na atazidi kuwafanyia wananchi kazi.

Jalang’o alisema kuwa huwa anakutana na wana Lang’ata nyanjani na anawaambia bila kubeta kwamba ameamua kufanya na rais kazi.

“Tunakutana nao kila siku tunafanya kazi, na hatujawahi zungumzia kwa sababu tunakutana nao kwenye mhadhara na nawambia nimeamua kufanya kazi na rais. Nawaambia hivi ndio mimi nimeamua.  Siku ya kupiga kura wataniuliza wewe tulikupa kazi na mimi nitawapa score card yangu,” Jalang’o alisema.