Ngesh Kaveve Kazoze atiririkwa na machozi ya furaha kuabiri ndege kwa mara ya kwanza

Hii ilikuwa mara yao ya kwanza kabisa katika maisha yao kuabiri ndege na pia kufika Mombasa na walimshukuru Mike Sonko kwa kufanikisha ndoto hiyo kutimia.

Muhtasari

• "Tunashukuru sana Sonko, tunajihisi faraja kubwa na tunasema shukrani kwa kutulipia shoo huko Mombasa na kutulipia nauli kwa ndege,” walisema.

Spider Clan wafika Mombasa kwa mara ya kwanza
KAVEVE KAZOZE Spider Clan wafika Mombasa kwa mara ya kwanza
Image: Screengrab

Mwanasiasa na mfanyibiashara Mike Sonko amewatimizia ndoto ya muda mrefu wasanii chipukizi kutoka kikundi cha Spider Clanmaarufu Kaveve Kazoze kwa kuwapeleka Mombasa kwa usafiri wa ndege.

Sonko alikutana na vijana hao mapema wiki jana katika ofisi yake ambapo aliwakung’uta mavumbi kwa kuwavisha upya katika muonekano wa kisupastaa.

Katika mkutano wao, Sonko aliweka wazi kwamba kando na kuwavisha vizuri, aiwapa kiasi kidogo cha hela na pia kuwapa ahadi ya kuwapeleka Mombasa, Shanzu kutumbuiza katika klabu yake ya Strehe, Club Volume wikendi hii.

Kwa kutimiza neno lake, Ijumaa aliondoka nao kutoka Nairobi kwa usafiri wa ndege kwenda Mombasa na vijana hao hawakuweza kuzuia hisia zao na faraja kwa Sonko.

Walifunguka kwamba ndio mara yao ya kwanza kabisa kuabiri ndege lakini pia ndio mara ya kwanza katika maisha yao kwenda Mombasa, jiji la pili kwa ukubwa Kenya lililoko katika mwambao wa Pwani ya Bahari Hindi.

“Ndio mara ya kwanza tunaenda Mombasa na kupanda ndege pia. Watu wa Mombasa. Tunashukuru sana Sonko, tunajihisi faraja kubwa na tunasema shukrani kwa kutulipia shoo huko Mombasa na kutulipia nauli kwa ndege,” walisema.

Ngesh aliyekuwa mnyamavu katika mahojiano hayo kwa kuzindiwa na hisia alisema kwamba urafiki wake na Manzi wa Kibera ulianza Nairobi na amekuwa akimshika mkono pakubwa kumwelekeza katika chochoro za hapa na pale.

“Manze mashabiki wa Mombasa tunakuja huko hivo Shanzu tunakuja huko. Tuna kazoze ya hiyo side hii wikendi unakuja mapema unapata tikiti. Sisi tuko tayari na kila kitu kuchukua video za challenge,” Ngesh wa Vasha alisema.