Unadhalilisha muziki wa Tz kwa kuimba za wenyewe - Alikiba ampiga Diamond K.O

"Acha kukurupukia vya bwerere vilivyoundwa kazi yako ni kuiba tu, kaa chini, umiza kichwa ili upate chako original na kilicho bora," Alikiba alimzomea Diamond.

Muhtasari

• Alimtaka Diamond na wenzake kuacha kukurupukia vilivyoundwa na badala yake kuumiza vichwa ili kupata vilivyo bora na asilia.

Alikiba amtupia bomu la moto Diamond kisa wimbo wa kura
Alikiba amtupia bomu la moto Diamond kisa wimbo wa kura
Image: FACEBOOK, INSTAGRAM

Huku Diamond akiendelea kuteketezwa vikali na raia wa Nigeria mitandaoni kwa tuhuma za kuwa na mazoea ya kuimba sehemu ya idundo ya ngoma za wasanii wao, wasanii wa nyumbani pia hawajaachwa nyumba.

Diamond yuko chini ya shinikizo kufuta wimbo alioshirikishwa na Juma Jux, ‘Enjoy’ ikiwa ni chini ya wiki moja tu baada ya kuutoa kutokana na Wanigeria kudai kwamba mdundo wa wimbo huo umeigwa kutoka kwa mdundo wa ngoma ya ‘Who’s your guy’ yake Spyro na Tiwa Savage iliyotoka miezi mitano iliyopita.

Nchini Tanzania, lehendari wa muziki wa kizazi kipya ambaye anatajwa kuwa adui wa muda mrefu wa Diamond, Alikiba naye ametia neno kwenye mjadala huo mkubwa ambao umesambaa mitandaoni kumtaja Diamond kama msanii mwenye hulka ya kuchukua midundo ya wasanii wenzake.

Kupitia ukurasa wa Twitter, Alikiba alimwambia Diamond kwamba nia yake ni nzuri kuupaisha muziki wa Bongo Fleva kimataifa lakini wakati huo huo pia anaudhalilisha muziki wao kwa kufanya wizi wa midundo pasi na kuwa na maelewano na wasanii wenyewe wa ngoma hizo.

Alikiba alimshauri ‘bwana mdogo kwevo’ kuwa na utaratibu na mwenye mdundo kabla ya kutumia mdundo huo ili kuepuka masimango ya kuburuzwa mitandaoni kwa wizi wa kazi zilizo na hakimiliki.

Alimtaka Diamond na wenzake kuacha kukurupukia vilivyoundwa na badala yake kuumiza vichwa ili kupata vilivyo bora na asilia.

“Tunadhalilisha muziki wa TZ na kufanya plagiarism. Umizeni vichwa vijana. Sampling ni vizuri lakini si kuimba, hapana kwa kweli,” Alikiba alituma ujumbe wake kwa Diamond.

Kwenye mtandao wa Instagram, Watanzania wengine waliendelea kuonesha chuki yao kwa Diamond wakisema kuwa halikuwa wazo la Jux ambaye wimbo ni wake kuiba iwmbo huo bali Diamond kwa vile ana historia ya nyuma kutuhumiwa kuiba ndiye huenda alimuingiza Jux kwenye chaka hilo.

“Jux naamini haikuwa idea yako kuiba hii Enjoy kwa Wanigeria, niko na uhakika hili lilikuwa wazo la Diamond na ndio kakuingiza kwenye chaka,” Mange Kimambi mkosoaji mkali wa Diamond aliandika.