Aslay afichua kwa nini hata kwa mtutu wa bunduki hawezi fanya muziki wa Amapiano

"Hata nikiimba Amapiano naona kabisa ni kama najishobokesha sehemu ambayo sipo, uongo dhambi,” - Aslay.

Muhtasari

• Aslay alitumia pia nafasi hiyo kuwashauri wenzake kina Diamond na Alikiba ambao wanazidi kutupiana mikwara.

Aslay afunguka kwa nini hawezi imba Amapiano.
Aslay afunguka kwa nini hawezi imba Amapiano.
Image: Instagram

Msanii Aslay amefunguka kwa upana ni kwa nini hahisi kama ipo siku atakuja kukaa na kukumbatia wimbo la muziki wa Amapiano wenye asili ya Afrika Kusini.

Katika mahojiano kwenye kituo cha rdio cha East Africa, Aslay alisema kwamba yeye muda wote anajiona kuwa Bongo Fleva, na ni kampeni ambayo ameianzisha na anatumai kuiendeleza kwa mikoa Zaidi ya 23 kutangaza kuwa yeye ni Bongo Fleva.

Hata hivyo, msanii huyo alisisitiza kwamab kujitenga kwake na muziki wa Amapiano ambao umekumbatiwa pakubwa na wasanii wengi wa Bongo hakuna maana kwamba anachukia midundo hiyo ya Afrika Kusini.

“Sisemi hivyo kama labda niachukia Amapiano. Mimi kusema ukweli Amapiano siwezi. Sidhani kwa sababu sasa hivi nina wazo langu la ‘mimi ni bongo fleva’ yaani kitu ambacho nakitengeneza sasa hivi, labda kama kuna wadogo zangu watakaokuja wajue kwamba kwenye bongo fleva na mimi pia nipo,” alisema.

“Mimi bado nitaendelea kukwama hapa kwa bongo fleva kwa sababu ni muziki ambao hata nikiimba Amapiano naona kabisa ni kama najishobokesha sehemu ambayo sipo, uongo dhambi,” aliongeza.

Aslay alitumia pia nafasi hiyo kuwashauri wenzake kina Diamond na Alikiba ambao wanazidi kutupiana mikwara na vijembe, akiwaambia kwamba wanapoendelea kukiwasha kwenye Amapiano pia wasisahau muziki wa Bongo fleva.

“Amapiano sio muziki mbaya kusema labda tuutukane. Wenzetu ambao wanatupiana maneno wanasema labda ndio muziki ambao uko kwenye kasi inayotakiwa lakini pia tusisahau Bongo Fleva yetu ambayo imetufanya sisi tutambulike huku nje. Kwa hiyo kama tunafanya Amapiano tujitahidi pia na kuweka vibongo fleva viwili vitatu ndani ya hizi Amapiano,” Aslay alishauri.