Zuchu alia akifanya video bila 'filters' kuwajibu wanaokejeli ngozi yake

“Mimi si mdoli na naweza kuwa na madoa meusi hapa na pale lakini hiyo ni kazi inayoendelea. Huwa sijali kabisa kama mnafikiria ngozi yangu si nzuri kuwaridhisha nyinyi"

Muhtasari

• “Kama unahisi ngozi yangu si nzuri vya kutosha kukufurahisha wewe, hilo ni tatizo lako."

• Kama unahisi hupendi mwili wangu, mimi wala sijali, najipenda mwenyewe, sina ubaya"

Zuchu awajibu wanaokejeli ngozi ya rangi yake.
Zuchu awajibu wanaokejeli ngozi ya rangi yake.
Image: INSTAGRAM

Msanii wa WCB Zuchu ameamua kunyoosha maelezo kuhusu ngozi yake na safari hi amerekodi video akiwakomesha wale wanaodhihaki ngozi yake kuwa ni mbaya.

Msanii huyo alirekodi video ambayo imepakiwa mitandaoni akituma ujumbe wake kwa wabaya wake na kusema kwamba si lazima kila mtu amchukulie kuwa yeye ni mtu mwenye ngozi laini, kwani yeye ni binadamu na anaweza kuwa na madoa meusi lakini anaendelea kuilinda ngozi yake.

“Hii video iwaendee watu wote mlionidhihaki kuhusu ngozi yangu. Sasa kama ambavyo mnaweza kuona, hii ni video ni asili kabisa haina filters yoyote nimeichukua moja kwa moja kutoka kwa simu. Hapa mwilini nimepaka mafuta ya nazi na hii ndio ngozi yangu, nadhani ngozi yangu iko vizuri…” Zuchu alisema.

“Mimi si mdoli na naweza kuwa na madoa meusi hapa na pale lakini hiyo ni kazi inayoendelea. Huwa sijali kabisa kama mnafikiria ngozi yangu si nzuri kuwaridhisha nyinyi. Mimi nahisi ni binadamu, ninaweza kuwa na madoadoa machache na hiyo ni sawa kabisa,” aliongeza.

Zuchu pia alisema katika kipindi kichache amekuwa na uzoefu kutoka kwa mashabiki wake, amejifunza tofauti yake na wengi ni hii;

“Tofauti yangu ni nyinyi, mnahisi ili mtu kuwa na ngozi nzuri mpaka ajichubue. Tofauti yangu ni nyinyi ni kwamba mimi hupitia mchakato wa kiasili kulainisha ngozi yangu, au kidonda au kipele. Kwa hiyo huyu ni mimi, si mdoli na siwezi kuwa kama ambavyo mnataka na pia kujichubua mimi siwezi,” Zuchu aliwaacha waliomsimanga na tope lao usoni.

Kwa maoni yake, Zuchu anahisi kwamba mtu ambaye anajichubua hajipendi na wengi wanaomtaka kujichubua ili kupata ngozi laini ni Dhahiri hawajipendi.

“Kama unahisi ngozi yangu si nzuri vya kutosha kukufurahisha wewe, hilo ni tatizo lako. Kama unahisi hupendi mwili wangu, mimi wala sijali, najipenda mwenyewe, sina ubaya wa kashifa wala huo uzuri wa sifa sitaki. Nina ujasiri katika mwili wangu mwenyewe,” alisema.