Cassypool adai Daimond Platinumz ndiye chanzo cha muziki wa Kenya kudorora

'Diamond ameharibu muziki wa Kenya kupitia ushirikiano wake na watangazaji fulani hapa nchini," Cassypool alidai.

Muhtasari

• Cassypool sasa alidai kuwa mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, Diamond Platinumz amehusika pakubwa na kuharibu muziki wa Kenya.

• Cassypool pia alisema kwa ujasiri atakuwa Rais wa Kenya baada ya Rais William Ruto kustaafu mwaka wa 2032.

Aliyekuwa mgombea wa Urais,Cassypool adai Diamond ndiye chanzo cha muziki wa Kenya kudorora.
Aliyekuwa mgombea wa Urais,Cassypool adai Diamond ndiye chanzo cha muziki wa Kenya kudorora.

Mwanasiasa na sosholaiti Kevin Onyango almaarufu Cassypool sasa amedai kuwa mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, Diamond Platinumz amehusika pakubwa na kuharibu muziki wa Kenya.

Mwanasiasa huyo ambaye amewai wania kiti cha Urais nchini, alibainisha kuwa hakuwa na tatizo lolote na muziki kutoka nchini jirani ya Tanzania japo tu alikuwa na tatizo na mmiliki wa lebo ya Wasafi.

"Diamond nina tatizo na yeye. Na ata Wasafi wanajua nina tatizo tu na huyo dogo sina issue na watanzania. Tatizo langu ni kuwa Diamond ameharibu muziki wa Kenya kupitia ushirikiano wake na watangazaji fulani hapa nchini."

Cassypool alifichua sababu kuu ya matatizo yake na baba huyo wa watoto wanne ni kuwa anafanya wimbo ambazo kwake hazielimishi ama hazina umuhimu wowote kwa wasikilizaji na wafuasi wake.

"Mimi nampiga vita kwote, na ndio maana juzi nikasifia wimbo wa Alikiba lakini hii nyimbo yake hapana. Wimbo huo sasa una ujumbe gani kwa wasikilizaji kusema tu ukweli. Wimbo unaitwa sumu. Sumu si inaleta kifo na kuleta magonjwa."

Katika mahojiano hayo hayo na mwandishi wa habari wa Mpasho, Dennis Milimo, Cassypool alisema kwa ujasiri kuwa atakuwa Rais wa Kenya baada ya Rais William Ruto kustaafu mwaka wa 2032.

"Tafadhali, take note of this, baada ya Rais William Ruto, rais atakaye fuata ni Kevin Odhiambo Onyango."

Wakati huo huo, Cassypool alimfichulia Milimo Kuwa anakodolea macho nafasi ya mshauri wa rais katika serikali ya Kenya Kwanza.

" Mwaka ujao ninataka kumfanyia kazi Rais William Ruto. Niligombea kiti cha urais mwaka wa 2022 na kwa hivyo nafasi hii  ya kuwa mshauri wa Rais inalingana na utaalam wangu."