Nimebeba tasnia ya muziki nchini peke yangu kuanzia kitambo- Willy Paul ajigamba

Willy Paul amemjibu mwimbaji mwenzake, Bahati ambaye alikuwa akiwataka wanamuziki wa Kenya kuamka.

Muhtasari

• Kulingana na Pozee, muziki wake ndio wa pekee unaotambuliwa nje ya mipaka ya Kenya na hivo kujitwika taji la mwanamuziki bora nchini.

• Willy Paul aliwahakikishia mashabiki wake kuwa atarejea katika ubora wake hivi karibuni bila msaaada wa mwanamuziki yeyote.

Image: INSTAGRAM// WILLY PAUL

Willy Paul amemjibu mwimbaji mwenzake Kelvin Kioko almaarufu Bahati ambaye alikuwa akiwataka wanamuziki wa Kenya kuamka na kuimarisha kazi yao ili kupigania nafasi katika muziki wa ukanda wa Afrika Mashariki.

Pozee alidai kuwa kwa muda mrefu amekuwa akiubeba muziki wa Kenya nje na ndani ya Kenya. Kulingana naye, muziki wake ndio wa pekee unaotambuliwa nje ya mipaka ya Kenya na hivyo kujitwika taji la 'mwanamuziki bora nchini.'

"Sijakuja hapa kupigana na yeyote ila tukusema ukweli uliopo. Nimeibeba tasnia ya muziki nchini peke yangu kuanzia kitambo."

Mmiliki huyo wa lebo ya Saldido Records alieleza masikitiko yake na blogu za Kenya akidai zilikuwa zikiwamiminia sifa wasanii ambao hawakustahili na kudai wao ndio wa kulaumiwa kwa kudorora kwa muziki wa Kenya.

“Huku nyumbani mnasifia artists that make no sense and has no humour. Katika kazi zao, Mablogu za huku nchini zimechangia asilimia 100 kuharibu sekta yetu kwa kuunga mkono kazi duni na wanamuziki wa kigeni.”

Baba huyo wa watoto wawili aliwahakikishia mashabiki wake kuwa atarejea katika ubora wake hivi karibuni bila msaaada wa mwanamuziki yeyote.

Jumatatu, Bahati alijitokeza na kuwataka wasanii Wakenya kuamka na kuimarisha kazi yao ili kupigania nafasi yao katika muziki wa ukanda wa Afrika Mashariki.

Mpenzi huyo wa Diana Bahati, katika taarifa yake ya Jumapili jioni alifafanua kuwa muziki kutoka kwa majirani wetu Watanzania umeendelea kutupiku kwa kiwango kikubwa kwa muda sasa.

“Wasanii wenzangu wa Kenya, tunaweza jaribu kupuuza hili lakini ukweli ni kuwa tumeacha jirani analala hadi na bibi zetu. Kuanzia Youtube, Boomplay, Itunes hadi kwa redio na runinga zetu.” ilisoma ujumbe huo wa Bahati.

Baba huyo wa watoto wanne, alieleza masikitiko yake baada ya kufika katika mtandao wa YouTube na kupata nyimbo za wasanii kutoka nchi ya Tanzania zikiongoza orodha ya nyimbo zinazovuma sana nchini Kenya, kuanzia nambari ya kwanza hadi nambari ya 10.