Ruto anunua mahindi choma kwa shilingi laki moja taslimu kutoka kwa hasola wa Mombasa

Baada ya kukabidhiwa mahindi hayo, rais aliyashambulia kwa haraka huku pia akimtaka mchuuzi huyo kumpa gavana Nassr mahindi choma moja pia.

Muhtasari

• Rais alimuamrisha msaidizi wake kumkabidh shilingi elfu mia moja taslimu kutoka kwa mkoba ndani ya gari lake ili kununua mahindi.

Ruto anunua maindi kwa laki moja.
Ruto anunua maindi kwa laki moja.
Image: Screengrab

Rais William Ruto Alhamisi alianza ziara ya siku chache katika eneo la mwambao wa Pwani ya kenya.

Katika mizunguko yake akiongozana na gavana wa kaunti hiyo Abdulswamad Sherrif Nassir, mbunge wa Nyali Mohammed Ali miongoni wa viongozi wengine, alifika katika eneo la Mama Ngina Drive ambapo aliwapata mahasola wakifanya biashara ndogo ndogo za kutafuta unga.

Miongoni wa wafanyibiashara hao, Ruto alifurahishwa na wanaume waliokuwa wakifanya biashara ya kuchuuza mahindi choma na kina mama ambao walimwambia wanajitafutia riziki katika kuchuuza maji ya kunywa pamoja na vinywaji vingine vya kujiburudisha.

Rais alimuamrisha msaidizi wake kumkabidh shilingi elfu mia moja taslimu kutoka kwa mkoba ndani ya gari lake ili kununua mahindi.

Katika video ambazo zimeenezwa mitandaoni, Ruto alitoa bunda la noti za shilingi elfu 100 na kumkabidhi muuza mahindi choma huku watu wakimshabikia kwa mbwembwe.

“Nani mwenyekiti wa hii soko, elfu mia moja ndio hii patia hawa watu,” Ruto alisema huku akitoa hela hizo kwenye bahasha na kumkabidhi jamaa aliyetambuliwa kama mwenyekiti wa soko hilo.

Baada ya kukabidhiwa mahindi hayo, rais aliyashambulia kwa haraka huku pia akimtaka mchuuzi huyo kumpa gavana Nassr mahindi choma moja pia.

Hii si mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa taifa kuonesha mapenzi yake kwa wafanyibiashara wa chini. Itakumbukwa mapema mwaka huu wakati wa kuzindua mkopo wa Hustler Fund, Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua pia walionekana wakinunua na kufurahia mahindi choma kutoka kwa hasola mmoja aliyekuwa katika maonesho ya uzinduzi wa mkopo huo unaonuiwa kuwasaidia wafanyibiashara wadogo kujiinua na kujikimu kimaisha.