Ukiona nimetoa ngoma yoyote funga mdomo, najua ninachofanya - Diamond kwa Alikiba

“Unapoona nimetoa ngoma yoyote, funga mdomo, maana sikurupuki, naachia ngoma kwa mkakati maalum,” Diamond alimfokea Alikiba.

Muhtasari

• Diamond aliburuzwa pakubwa kwa kusemekana kuwa alichukua baadhi ya midundo ya nyimbo za wasanii wa Nigeria.

• Diamond alijipiga kifua akisema kuwa huwa hakurupuki tu bora kutoa muziki, bali huwa na utaratibu na mikakati yake ambayo anazingatia kabla ya kuachia dude jipya.

Diamond amfokea Alikiba.
Diamond amfokea Alikiba.
Image: Instagram

Ugomvi wa Diamond na Alikiba unazidi kurindima mitandaoni huku sasa Simba akimtaka Alikiba kufyata ulimi wake kuhusu kumpa ushauri Diamond jinsi ya kufanya muziki.

Kupitia Instastoy yake, Diamond amejivunia jinsi wimbo wake wa My Baby akimshirikisha Chike unavyozidi kufanya vizuri haswa nchini Nigeria, taifa ambalo linatajwa kuwa ngome ya miziki ya kizazi kipya barani Afrika.

Diamond alijivunia wimbo huo jinsi ulivyopata mapokezi makubwa ikiwa ni chini ya wiki tatu tu yangu kuuachia na kumtaka Alikiba – japo hakumtaja moja kwa moja – kunyamaza kabisa pindi anapoona Diamond ametoa wimbo, kwani ana mpango wake na anajua anachokifanya.

Diamond alijipiga kifua akisema kuwa huwa hakurupuki tu bora kutoa muziki, bali huwa na utaratibu na mikakati yake ambayo anazingatia kabla ya kuachia dude jipya.

“Unapoona nimetoa ngoma yoyote, funga mdomo, maana sikurupuki, naachia ngoma kwa mkakati maalum,” Diamond alifoka.

Wiki jana, Alikiba alimkosoa vikali Diamond kwa jinsi alivyofanya wimbo wake alioshirikishwa na Jux, Enjoy, akisema kwamba msanii huyo anaudhalilisha muziki wa Bongo Flava kwa kile alichokiita ni wizi wa kazi za Sanaa za wasanii wa Nigeria.

Diamond aliburuzwa pakubwa kwa kusemekana kuwa alichukua baadhi ya midundo ya nyimbo za wasanii wa Nigeria.

Blogu za Afrika Magharibi zilimvamia kama nzige na hata kutaja nyimbo zisizopungua tano za wasanii wao ambazo zilikuwa na mfanano kweney mdundo na nyimbo alizokuja kutoa nyuma Diamond Platnumz.

Lakini Spyro, msanii aliyesemekana kuibiwa mdundo na Diamond alivunja ukimya akiwanyamazisha watu kwamba hakuna mtu ambaye ni kisiwa duniani kiasi kwamba anaweza fanya jambo peke yake pasi na kupata ushirikiano wa wengine.

Aliwataka wamuache Diamond kupumua na kutompa shinikizo lisilo la maana kwamba anaiba midundo ya wasanii wengine.