Pozee amshukuru mamake kwa kumlea na tamaduni ya kutovaa mavazi ya kike

Hiki kilikuwa chuma cha moto ambacho kilielekezwa kama uchokozi moja kwa moja katika kambi ya Bahati ambaye amezua minong'ono mitandaoni kwa kuvaa mavazi ya kike.

Muhtasari

• Sio Lazima Nivae Skirt Ndio Nisikike, Kukaa Kweli Kwa Utamaduni Wangu Wa Kiafrika. - Willy Paul.

Pozee amshambulia Bahati.
Pozee amshambulia Bahati.
Image: Instagram

Vita vya kibabe kati ya wasanii Bahati na Willy Paul vinaendelea, na wawili hao wameendeleza mashambulizi dhidi ya mwingine kuhusu suala nyeti la kudorora kwa muziki wa Kenya.

Wiki moja iliyopita Bahati ndiye aliibua suala hilo akisema kwamba muziki wa Kenya umekuwa ukitegemea jitihada zake, jambo ambalo Pozee alikanusha akisema ni yeye amekuwa akiubeba muziki wa Kenya peke yake.

Sasa Pozee amerudi na kupiga tena pale kwenye mshono, safari hii akiingilia hulka ya Bahati ya kuvaa mavazi ya kike.

Pozee kwenye Instagram yake alipakia picha akipokelewa katika tafrija moja kaunti ya Bungoma na kusema kwamba alipokelewa kishujaa na watu wakampa masikio yao.

Msanii huyo wa kujitapa alimchokoza Bahati akisema kwamba yeye husikilizwa hata bila kuvalia nguo za kike, akisema kwamba tamaduni za Kiafrika siku zote mwanamume hafai kuvaa kama mwanamke – tamko lililolenga kwenye kambi ya Bahati.

Msanii huyo pia alimshukuru mamake Salome kwa kumlea yeye kwa desturi nzuri na misingi ya kujua jinsi mtoto wa kiume wa Kiafrika anastahili kuvaa.

“Usalama Kabisa, Asante Bungoma! Sio Lazima Nivae Skirt Ndio Nisikike, Kukaa Kweli Kwa Utamaduni Wangu Wa Kiafrika. Asante Salome Kwa Kumlea Mwanaume Halisi... Upendo Mmoja,” Pozee alisema.

Ikumbukwe Bahati amekuwa akigonga vichwa vya bahari baada ya kuonekana amevaa kama mwanamke wikendi iliyopita.

Katika video ambayo alipakia, Bahati alikuwa na mke wake Diana Marua na alikuwa amevalia rinda la rangi nyekundu, wigi kichwani na midomo yake alikuwa amejipodoa.

Watu vwamejitokeza kumkashifu wengine wakimtaja kuwa ameacha muziki na kugeukia katika ukuzaji maudhui kwa kufanya skits za kusisimua mashabiki wanaomfuata kwenye mitandao ya kijamii.

Miongoni mwa zogo hilo, msanii huyo aliibua jingine kuhusu muziki wa Kenya, akijiita kuwa mwokozi jambo ambalo Willy Paul amepinga vikalina hata juzi kwenye Instastory yake akimwambia ‘bosi wewe shikana na bibi yako’.