Mjukuu wa Kibaki amtetea mwanawe Uhuru, Jomo dhidi ya sakata la bunduki

Sean alisisitiza kwamba yeye hafikirii hata siku moja atakuja kujipata katika siasa za kenya akisema kwamba wanasiasa wameufanya kuwa mchezo mchafu zaidi usiotamanika.

Muhtasari

• “Jomo ni mtu ambaye ninamjua kibinafsi  na nafikiria alilengwa kinyume cha haki." - Sean.

Sean Andrew amtetea Jomo Kenyatta
Sean Andrew amtetea Jomo Kenyatta
Image: Instagram

Mjukuu wa rais wa tatu wa Kenya hayati Mwaic Kibaki, Sean Andrew amekuwa mtu wa hivi punde kutoa maoni yake kuhusu sakata linalomkumba mwanawe rais wa nne Uhuru Kenyatta, Jomo.

Akizungumza na waandishi wa habari za mitandaoni, Andrew alisema kuwa kwa maoni yake, anahisi sakata la bunduki linalozua joto la kisiasa kwa Jomo si la haki, na kuwa haifai aingizwe kwenye joto la kisiasa baina ya mirengo ya Azimio na Kenya Kwanza.

“Jomo ni mtu ambaye ninamjua kibinafsi  na nafikiria alilengwa kinyume cha haki. Mimi sitaki kuegemea upande wowote kisiasa lakini nafikiri Jomo hana hatia, pia Mama Ngina. Hawakufaa kumlenga mtu yoyote ambaye hahusiki katika kile ambacho wanatofautiana nacho,” Sean Andrew alisema.

Mjukuu huyo wa Kibaki alisisitiza kwamab viongozi hao – Uhuru, Raila na Ruto – ni watu wazima ambao wanafaa kuketi chini na kupata mwafaka kuliko kuendeleza tofauti zao za kisiasa kwa familia zao.

“Mimi nafikiri hawa ni watu wazima na wanafaa kusuluhisha tofauti zao. Hawafai kutuhusisha katika mambo ya maandamano au kitu chochote. Tuna masuala nyeti kama binadamu kama Wakenya, na nafikiri si vizuri kuwakusanya vijana wadogo kwenda kuandamana na kufa kwa kupigana na polisi, dola na vitu vingine,” alisema.

Alisema kwamab hata hivyo yeye asingependa sana kulivalia njuga suala la siasa humu nchini akisema kwamab yeye si mwanasiasa.

“Mimi siwezi kuingia katika siasa hata kidogo, hapa Kenya sidhani ni sharti mtu uwe mwanasiasa ili kuwahudumia watu hadharani. Nafikiri unaweza saidia idadi nzuri tu ya watu bila kuwa mwanasiasa. Siasa ni biashara chafu na kwa bahati mbaya wameifanya kuwa chafu Zaidi na sina nia yoyote katika hilo, ninaweza kuwahudumia watu kwa njia yangu tofauti,” Sean Andrew alisema.