Guardian Angel afunguka kuhusu kufungwa jela, kuishi mitaani akiwa mtoto

Mwimbaji Guardian Angel amedokeza kwamba alikuwa mvulana mtukutu sana katika enzi za utoto wake.

Muhtasari

•Guardian alifichua kwamba maisha yake ya utotoni kimsingi yalihusisha yeye kujaribu kujifunza jinsi ya kuishi peke yake.

•Guardian Angel amefichua amewahi kuishi mitaani, kufungwa katika seli na kupelekwa shule ya kurekebisha tabia katika siku za utotoni.

Image: INSTAGRAM// GUARDIAN ANGEL

Mwimbaji wa nyimbo za injili Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel amefunguka kuhusu kutokuwa na maisha ya kawaida ya utotoni kama watoto wengine wengi walivyokuwa.

Wakati akizungumza na Standard Entertainment & Lifestyle, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 35 ambaye amekuwa msiri sana kuhusu siku zake za utotoni alifunguka kuhusu baadhi ya masaibu ambayo alikumbana nayo alipokuwa akikua.

Guardian Angel alifichua kwamba maisha yake ya utotoni kimsingi yalihusisha yeye kujaribu kujifunza jinsi ya kuishi peke yake.

"Jinsi nilivyokua, na mambo mengi niliyofanya si kama maisha ya kawaida ambayo watoto huwa nayo wanapolelewa," Guardian Angel alisema.

Mwimbaji huyo alizungumza kuhusu kuishi mitaani, kufungwa katika seli na kupelekwa shule ya kurekebisha tabia katika siku za utotoni wake.

"Wakati fulani nililazimika kuishi mitaani, wakati fulani ilibidi niishi kwenye seli kwa mwezi mmoja au miwili. Wakati fulani ilibidi niende shule ya kurekebisha tabia. Baadaye niliishi na mama yangu kwa takriban miaka mitatu hadi minne kisha nikarudi kufikiria jinsi ya kuishi kama mwanaume,” alisimulia.

Mwimbaji huyo alifichua kuwa mapenzi yake kwa muziki yalianza akiwa mdogo sana na kudokeza kuwa hata akiwa mtoto alikuwa akiimba. Alisema kuwa alikuwa akishiriki tamasha la muziki na kucheza nyimbo na ala za muziki za asili,  jambo ambalo lilimsaidia sana katika kujenga sanaa yake ya muziki.

Guardian alisema hata hivyo hakuwahi kutarajia kuwa angekuwa mwimbaji wa nyimbo za injili na akafichua kwamba muziki wake wa kwanza ulikuwa wimbo wa mapenzi.

“Nilipoanza kuimba nilikuwa nafanya nyimbo za mapenzi. Wimbo wangu wa kwanza, hata sikumbuki chochote. Injili sasa ilitokea kwangu maana kwakua nilifika mahali nikamjua Mungu na kuamua kuzaliwa mara ya pili. Wakati ninaanza kuimba nilikuwa tayari nimezaliwa mara ya pili kwa hiyo nilikuwa na chaguo la kumuimbia Mungu tu. Ndivyo nilivyoanza kuimba injili,” alisema.

Mume huyo wa Esther Musila alidokeza kuwa tasnia ya injili nzuri alipojitosa ndani yake na alipata usaidizi uliohitajika.

Alisema ilimchukua takribani miaka mitano kupata wimbo wake wa kwanza mkubwa ambao ulimfungulia milango mingi katika tasnia ya muziki wa Injili.