Kajala na bintiye wajibu kilio cha Harmonize kwa kicheko cha dhihaka

Jumanne jioni Harmonize aliachia wimbo akiwasuta Kajala na bintiye kama matapeli waliomfyonza mali yake na kumuacha hoi, akitaja kwamba alimuachia gari aina ya Range na bintiye duka la mavazi.

Muhtasari

• Kicheko hicho bila shaka kimetafsiriwa kuwa mkuki wa kujibu mipigo katika kambi ya Harmonzie.

• “Nilidhani nimeyaona na kuyasikia yote. Wacha nicheke mie,”   Kajala aliandika kwenye video hiyo.

Harmonize na Kajala wapapurana,
Harmonize na Kajala wapapurana,
Image: Instagram

Mwigizaji mkongwe wa Bongo Movie, Fridah Kajala Masanja na bintiye Paula hatimaye wamezipata habari za Harmonize kuwasuta katika wimbo mpya, DeR Ex.

Harmonize aliachia wimbo huo jioni ya Jumanne na kwenye vesi msanii wa Konde Gang ametema makombora ya kashifa kwa hasira kwa Kajala ambaye ni mpenzi wake wa zamani.

Katika kile ambacho kimeonekana kama ni kujibu makavu ya Harmonize kwenye Dear Ex, Kajala na bintiye kama kawaida yao wamefanya video wakionekana kucheka kicheko cha dharau na kebehi.

Kicheko hicho bila shaka kimetafsiriwa kuwa mkuki wa kujibu mipigo katika kambi ya Harmonzie na Kajala kweney video hiyo ameandika kwamba wala hajashangaa kumsikia Harmonzie akilia, maana walijua kwa hali waliyomuacha nayo hangestahimili.

“Nilidhani nimeyaona na kuyasikia yote. Wacha nicheke mie,”   Kajala aliandika kwenye video hiyo.

Hii inakuja baada ya Harmonize kufunguka mengi kwenye wimbo huo jinsi alilazimika kumuachia Kajala gari alilompa kama zawadi ya kumrudia, aina ya Range lakini pia kumuachia bintiye Paula duka la bishara za nguo alilomfungulia wakati wa kilele cha mapenzi yao.

“Dear Ex, nimepata tetesi ya kwamba unanisema ili nionekane si mwema…. Kwangu kimya si ukilema ila nachunga vya kusema. Maana niliubeba msalaba nikawa mimi ndio baba na mama, nikajichanga tujaze kibaba,mbona husemi hayo?” Harmonize anaanza kwa cheche kali.

Harmonize anazidi kusema kwamba siku moja akija kulewa ataamua kumwaga mtama kwa kuku wengi ili nchi nzima ijue jinsi yeye Kajala na mwanawe walimtapeli vya kwake.

“Kiume nilishukuru nikapanguza makalio nikakuacha uende ukawe huru Range na Duka ni vyako… kama ulidhani nitafeli utangoja sana na siku nikilewa nitasema ukweli nchi ilivyoona matapeli. Sina hasira wala kinyongo na wala sipendi uongo wa vijembe na matongo ukitaka kutrend…” Harmonize anamvua nguo hadharani Kajala kwenye vesi ya pili.

Ama kweli hii vita haiku karibu na kutamatika na ndio mwanzo mashambulizi yanapangwa upya kutoka kwa kambi zote husika.