"Tunakosa kukubaliana sana!" Guardian Angel azungumzia kuwa chini ya usimamizi wa mkewe Esther Musila

Mwimbaji huyo alidokeza kuwa wakati mwingine huwa wanakuja na mawazo tofauti ambayo huwaacha wakikosa kuelewana.

Muhtasari

•Guardian Angel alidokeza kuwa sio kila wakati huwa anakubaliana na mke wake wanapokuwa wakifanya kazi pamoja.

•Guardian Angel alibainisha, muziki wake kumsaidia kupata mke ni mojawapo ya mafanikio makubwa katika taaluma yake.

Esther Musila na mume wake Guardian Angel
Image: INSTAGRAM// ESTHER MUSILA

Mwimbaji wa nyimbo za Injili Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel amefunguka kuhusu jinsi ilivyo kufanya kazi na mkewe Esther Musila kama meneja wake katika muziki.

Akizungumza na Standard Entertainment & Lifestyle, mwamamuziki huyo mwenye umri wa miaka 35 alidokeza kuwa sio kila wakati huwa anakubaliana na mke wake wanapokuwa wakifanya kazi pamoja.

Guardian alidokeza kuwa wakati mwingine huwa wanakuja na mawazo tofauti ambayo huwaacha wote wawili wakikosa kuelewana na kujadiliana hadi hatimaye kukubaliana.

“Tunatofautiana sana. Tunatofautiana sana lakini hasa kwa sababu tangu nimekuwa nikifanya hili kwa muda, kuna njia ambayo nadhani mambo yanapaswa kufanywa na pia yeye kuna njia ambayo anadhani mambo yanaweza kufanywa tofauti na jinsi nimekuwa nikifanya. Wakati huo tutakuwa na kutofautiana hapa na pale lakini mwisho wa siku tunapata kukubaliana na kutambua tunafanya jambo hili kwa upendo. Sote tunafanya hivyo kwa manufaa ya kujengwa kwa himaya yetu,” Guardian Angel alisema.

Mwanamuziki huyo alijivunia kufanya kazi na malkia huyo mwenye umri wa miaka 53 na akazungumza kuhusu umuhimu wa kuendesha lebo yake ya Seven Heaven Music pamoja naye.

Guardian Angel alibainisha kuwa kufanya kazi na Bi Musila ni tofauti na kuajiri mtu mwingine kutoka nje ya familia kwani mkewe anashikamana naye kila wakati, tofauti na wafanyikazi ambao wana uwezekano wa kukimbilia fursa bora wakati mambo yanapoharibika.

"Hatua ya mimi kufanya kazi naye ni kwa sababu aliona maono. Na amefanya maono yaonekane kama kitu ambacho yeye ni sehemu yake. Mara nyingi unapoajiri watu kutoka nje, wanafanya kazi. Mambo yakiharibika watahamia kwa msanii mwingine ambaye anafanya vizuri zaidi,” alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 35 alibainisha kuwa, muziki wake kumsaidia kupata mpenzi wake wa maisha ni mojawapo ya mafanikio makubwa katika taaluma yake.

"Kupitia moja ya nyimbo nilizofanya, niliweza kupata mpenzi," alisema.

Katika siku za nyuma, Musila amewahi kufichua kuwa wimbo wa Guardian Angel 'Rada' ulikuwa mwanzo wa muungano wao wa kudumu.

Mama huyo wa watoto watatu alisema alipata hamu ya kukutana na mwimbaji huyo baada ya kuusikia wimbo huo kwenye redio na kuupenda.

"Muungano wetu usingetokea kwa namna nyingine. Tulikuwa na mipango yetu lakini Mungu alitangulia mbele yetu na ameendelea kutuongoza katika safari yetu," alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Wawili hao walifunga ndoa mwanzoni mwa mwaka jana baada ya kuchumbiana kwa takriban maiaka miwili.