Karen Nyamu anyenyekea kuona matatu yenye picha yake nyumbani kwa kina Samidoh

Karen Nyamu na Samidoh wana watoto wawili na wamekuwa wakienda nyumbani kwa msanii huyo - Nyandarua - mara kwa mara japo hajamtambua rasmi kama mke wake wa pili.

Muhtasari

• “Ol Joro Orok, nawaona. Ahsante sana kwa upendo,” Karen Nyamu aliandika kwa unyenyekevu kwenye picha hiyo iliyomfurahisha na kumkosha.

• Gari hilo lilikuwa limebandikwa picha ya seneta Nyamu katika kioo cha nyuma.

Karen Nyamu atambuliwa nyumbani kwa kina Samidoh.
Karen Nyamu atambuliwa nyumbani kwa kina Samidoh.
Image: Instagram

Seneta Karen Nyamu ameshindwa kuficha furaha yake baada ya kuona gari la uchukuzi wa umma la kutoka nyumbani kwa kina baba wa watoto wake Samidoh likiwa limechorwa picha yake.

Seneta huyo alipakia picha ya gari hilo kwenye Instagram Story yake na kusema hachukulii kwa njia nyepesi mapenzi anayoonyeshwa na watu wa kutoka kwa kina Samidoh.

Matatu hiyo ya sacco ya Nyamakina ilipigwa picha ikiwa barabarani katika eneo ambalo Nyamu alisema ni kutoka Ol Joro Orok, kaunti ya Nyandarua – nyumbani kwa kina msanii maarufu wa Mugithi Samidoh.

Gari hilo lilikuwa limebandikwa picha ya seneta Nyamu katika kioo cha nyuma.

“Ol Joro Orok, nawaona. Ahsante sana kwa upendo,” Karen Nyamu aliandika kwa unyenyekevu kwenye picha hiyo iliyomfurahisha na kumkosha.

Kando na gari hilo, seneta huyo maalum ambaye hivi karibuni amekuwa akijitambua kama Mama Kanairo pia alioneshwa mapenzi kwa picha yake kuwekwa kwenye gari moja la uchukuzi wa umma pia katika eneo la Dagoretti Kusini, mtaani Kawangware.

Nyamu amekuwa katika uhusiano wa kimapenzi na Samidoh kwa miaka kadhaa sasa, ila sakata lao lilibainika mwaka 2021 Samidoh alipojitokeza hadharani na kuomba msamaha kwa mkewe Edday Nderitu akikiri kwamba amekuwa katika uhusiano wa kimapenzi wa siri na mwanasiasa huyo na hata kuzaa naye mtoto mmoja.

Miezi michache baada ya kukiri na kumuomba mkewe msamaha, Samidoh tena alijipata ameshindwa kuyakwepa mapenzi ya Nyamu ambapo mwaka jana walizaa pamoja mtoto wa pili.

Tangu kipindi hicho, mgogoro wa kimapenzi baina ya Karen Nyamu, Samidoh na mkewe wa kwanza u umekuwa ukigonga vichwa vya habari huku wengi wakiona sakata lao kama sarakasi.