Diamond atamani kupiga shoo na Alikiba na Harmonize kwenye jukwaa moja Wasafi Festival

“Watu watafurahi kuona shoo moja nikiwa mimi na yeye [Alikiba], itakuwa safi sana. Pia tupate mtu kama Konde, eeh bwana unajua lazima tutumie akili... kuna wakati wa comedy na kuna wakati wa kazi."

Muhtasari

• “Sisi kama Wasafi Festival tunapenda tushirikiane na kila mtu… ikimpendeza Alikiba pia tungependa tuwe naye" - Diamond.

• Wasafi Festival itaanza siku chache zijazo na watazunguka katika mikoa tofauti tofauti.

Harmonize, Alikiba na Diamond
Harmonize, Alikiba na Diamond
Image: Instagram

Msanii Diamond amefunguka matamanio yake makubwa ni kufanya shoo katika jukwaa moja la Alikiba na Harmonize mweiz huu wa Agosti wakati wa tamasha la Wasafi katika mikoa tofauti tofauti.

Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari kuhusu mipango na ratiba ya Wasafi Festival ambayo itang’oa nanga siku chache zijazo, Diamond alisema kwamba mambo ya kuoneshana kama kuna uhasama yabakie tu kwenye muziki lakini pale yeye alikuwa anazungumza kama mkurugenzi mtendaji wa Wasafi.

Alisema kwamba kabla ya tamasha hilo, atatoa ngoma na kakake Alikiba, Abdukiba na kusema kwamba ingempendeza sana iwapo Alikiba atakuwepo pia kwenye tamasha na angalau kushiriki naye japo kidogo tu.

“Sisi kama Wasafi Festival tunapenda tushirikiane na kila mtu… ikimpendeza Alikiba pia tungependa tuwe naye, unajua yaani ibaki huko mambo mengine lakini huku shughuli ziendelee. Ndio Wanigeria wanafanya hivo. Sisi tutafarijika sana tukiwa naye tukafanya shughuli pamoja pale. Unajua Alikiba si msanii mdogo ni msanii mkubwa na inawezekana yuko bize lakini ikiwezekana akatupa muda wake kidogo tutashukuru,” Diamond alisema.

“Watu watafurahi kuona shoo moja nikiwa mimi na yeye [Alikiba], itakuwa safi sana. Pia tupate mtu kama Konde, eeh bwana unajua lazima tutumie akili kwenye vitu tunavyovifanya. Kuna wakati wa kufanya comedy halafu kuna wakati sasa wa kufanya vitu vya Kiinchi. Mwisho wa siku sisi wote ni wamoja,” aliongeza.

Wasanii hao watatu wamekuwa wakiparurana mitandaoni mpaka kuwaaminisha mashabiki wao kwamba wao ni maadi wakubwa wasioweza kuonana ana kwa ana.

Wiki jana, Alikiba na Diamond walichemsha genge mitandaoni kwa kutukanana vibaya kiasi kwamba baadhi walihisi ugomvi wao umechanua hadi kileleni.

Lakini Diamond ambaye ni mujongeaji sana ameonekana kuashiria kwamba hakukuwa na ubaya wowote bali walichokuwa wakikifanya ni kutia uchachu kwenye tasnia ya Bongo Fleva ambaye alisema ilikuwa imelala kabla ya chokoza chokoza hizo.

Hata hivyo, Alikiba ambaye ni msiri na mkimywa hajaonekana kushuka na kulichukulia suala hilo kimzaha kama ambavyo Diamond amelichukulia.