DJ Fatxo afichua kufungua redio ya Kikuyu nchini Uingereza

Muhtasari

• Fatxo aliwataka wanablogu pia kujaribu kuwa na utu kidogo katika kazi yao licha ya kwamba simulizi zenye uchachu ndizo huuza.

• Msanii huyo pia alipata kuzungumzia maisha ya kifahari aliyokuwa akionesha katika kurasa zake mitandaoni akiwa nchini Uingereza.

DJ FATXO.
DJ FATXO.
Image: FaCEBOOK

Msanii wa Mugithi DJ Fatxo amefichua kuhusu ziara yake ya muda mrefu nchini UIngereza, ambapo amekuwa kwa wiki kadhaa na kurejea nchini wikendi iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari za mitandaoni pindi baada ya kutua JKIA, Fatxo alifichua kwamba kwa kushirikiana na meneja wake aliyeko nchini Uingereza, wanatarajia kuanzisha kituo cha redio cha kwanza kabisa ambacho kitakuwa kinapeperusha huduma zake kwa lugha ya Kikuyu.

“Meneja wangu anaitwa John Smith na anachukua nafasi ya fursa kubwa Uingereza na kusema kweli tuna mradi wa kufungua kituo cha redio na yeye, redio ya kwanza ya Kikuyu na ya Mwafrika nchini Uingereza,” Fatxo alifichua.

Msanii huyo pia alipata kuzungumzia maisha ya kifahari aliyokuwa akionesha katika kurasa zake mitandaoni akiwa nchini Uingereza.

Alisema kwamba magari yote yenye hadhi ya nyota tano aliyokuwa akionekana nayo katika mitaa na barabara za Uingereza ni ya meneja wake John Smith.

Fatxo alisema baada ya kurejea nchini, ataanzia pale alikoachia, akisema kwamba tangu azingirwe na sakata la kesi ya mauaji, alichukua likizo kidogo kuachia muziki na msisimko katika tasnia ya Mugithi umetokomea.

Msanii huyo alisema kwamba wiki kesho ataachia wimbo wake mwingine ambao utakuwa ni collabo kama njia moja ya kuonesha kwamba Duke wa Mugithi amerejea, kama anavyopenda kujiita.

Fatxo aliwataka wanablogu pia kujaribu kuwa na utu kidogo katika kazi yao licha ya kwamba simulizi zenye uchachu ndizo huuza.

“Nyinyi pia mkifanya hii kazi yenu jaribu kutenda sawa kidogo, tuchunge tusiangamize wengine tukijaribu kutafuta wengine tuangamize wenye hata hawana dhambi, tuangalie tu juu hakuna kitu cha maana kama kuwa hai,” aliwaambia.