Eric Omondi anamtafuta msichana aliyewapa makavu ana kwa ana viongozi wa Uasin Gishu

Msichana huyo aliyeonekana kujawa na ghadhabu aliwaambia viongozi hao kwa hisia kwamba haogopi kitu hata kama watataka kutuma wahuni ili kumdhuru.

Muhtasari

• Kaunti ya Uasin Gishu imekuwa ikikumbwa na skendo ambapo uongozi uliopita unadaiwa kuwalaghai wazazi mamilioni ya pesa ili kupeleka watoto wao Ufini kwa ajili ya masomo.

Eric Omondi amtafuta binti mjasiri
Eric Omondi amtafuta binti mjasiri
Image: Screengrab, Facebook

Mchekeshaji aliyekengeuka na kuwa mwanaharakati wa haki za ninadamu Eric Omondi ameonesha nia yake ya kukutana na msichana aliyeshabikiwa mitandaoni baada ya video yake kuibuka akiwapa makavu viongozi wa kaunti ya Nandi kuhusu sakata la kuwapeleka wanafunzi kuendeleza masomo yao Ufini.

Omondi kupitia ukurasa wake wa Instagram alichapisha sehemu ya video hiyo msichana huyo mjasiri akiwazomea viongozi wa kaunti ya Nandi na kusema kwamba angependa kukutana naye kwa haraka.

Omondi ambaye amekuwa pia akiendeleza vuguvugu la vijana kujikomboa kutoka uongo wa viongozi wa serikali alisema kuwa msichana huyo anawiana na ajenda zake za vijana kujitokeza bila kupepesa jicho na kuwaambia viongozi ukweli ili kujikomboa.

“Namtafuta Huyu Binti Haraka!!! Yeyote mwenye Mawasiliano yake tafadhali DM🙏🙏. WAKATI WETU NI SASA!!! Hakuna mtu atakayetuokoa, ikiwa hatutajiokoa wenyewe. TUNA MPANGO!!!” Eric Omondi alisema.

Msichana huyo ambaye alionekana kuwa na majungu aliwazomea viongozi hao akiwemo gavana Jonathan Bii, Seneta Jackson Mandago [ambaye ni gavana wa zamani] na naibu gavana wa sasa Barorot.

Alianza kwa kuwauliza mbona walichelewa katika mkutano huo ambao walikuwa wamewaambia wazazi na wanafunzi waliochania fedha zao waakti wa uongozi wa Mandago ili kufadhili masomo ya wanao nchini Ufini.

Pia alikwenda mbele kwa kuwauliza maswali magumu mbele ya kila mtu iwapo wanao walikuwa kweney ukumbi huo na iwapo wanajua dawa yoyote ya kupunguza makali ya msongo wa mawazo – swali ambalo wote walijibu hawajui na msichana huyo akawaambia kwamba wazazi wengi wanatumia dawa hizo kutokana na madhira ambayo uongozi wa kaunti umewaletea.

“Hii serikali ya Ruto ilikuwa ya mahasola, lakini mimi ninauza uji hali ya kuwa nimehitimu. Nilikuwa nafaa kwenda Kanada… nyinyi mnatudanganya sana, ni sawa hata kama mtatuma watu wenu waniuwe hata sina cha kuishi…” mrembo huyo alisema katika sehemu ya video hiyo yenye hisia.