Haitawahi kutokea mimi kufanya shoo moja na Diamond, asiwadanganye - Harmonize

Jumanne, Diamond alionesha matamanio yake ya kujumuika na Harmonize kwenye jukwaa moja kwa ajili ya shoo, haswa haswa huko kwao Harmonize, Mtwara.

Muhtasari

• “Najua mna mioyo safi sana, hakikisha mnaenda kumuunga mkono ila suala la mimi kuwepo halitokuja kutokea,” alisisitiza.

Diamond na Harmonize
Diamond na Harmonize
Image: Screengrabs: YouTube

Harmonize, msanii kutoka lebo ya Konde Music Worldwide amefutilia mbali uwezekano wa kufanya shoo kwenye jukwaa moja na aliyekuwa baba yake katika tasnia ya muziki, Diamond Platnumz.

Harmonize amenyoosha maelezo haya muda mfupi baada ya Diamond kusema kwamba anatamani sana kufanya shoo kwenye jukwaa moja na Harmonize katika tamasha lake la Wasafi litakalong’oa nanga hivi karibuni.

Harmonize amesema kwamba Diamond anatamba uongo kwamba anatamani kufanya shoo na yeye kwa sababu anajua akisema hivyo watu wa Mtwara – nyumbani kwa kina Harmonize watajitokeza kwa wingi, lakini akasema kwamba suala hilo halitokuja kutokea katika maisha yake.

“Watu wangu wa Mtwara, sitokuwepo na haitotokea, asiwadanganye. Lengo lake anataka kujaza uwanja ili achambe. Sisi tumeshajaza kwao tayari,” Harmonize alisema kupitia Instastoy yake.

Msanii huyo hata hivyo aliwarai watu wa nyumbani kwake kujitokeza kwa wingi ili kumpac shavu chale wake wa zamani akisema kwamba anajua hawatomuangusha.

“Najua mna mioyo safi sana, hakikisha mnaenda kumuunga mkono ila suala la mimi kuwepo halitokuja kutokea,” alisisitiza.

Jumatatu wakati wa mkutano na vyombo vya habari, Diamond alisema kwamba maandalizi ya Wasafi Festival yanaendelea vyema na wameamua kuanzia katika mkoa wa Mtwara – ngome ya Harmonize kimuziki.

Mkurugenzi huyo wa Wasafi alisema kwamba anatamani sana kuwaona wasanii kama Alikiba na Harmonize kwenye tamasha hilo na hata kupanda kwenye jukwaa ili kukiwasha pamoja, akisema kwamba uhasama ubakie kule nje lakini likija ni suala la kuunganisha nchi, basi wote wanafaa kujumuika pamoja.