Anjella akiondoka nilimwambia Harmonize amuachie hata gari akakataa - Kajala

"Mimi ndio mtu wa kwanza hata nilikuwa namwambia Harmo [Harmonize] Anjella ni mtu ambaye anaumwa yaani ikiwezekana muachie hata gari aende nalo" - Kajala.

Muhtasari

• “Nilivyoona ile video mwenyewe I was like… yaani sijui labda mtu mwenyewe unaona upepo unavyoenda na wewe unaamua kuufuata," - Kajala.

Kajala ashangazwa na Anjella kumdhihaki kwenye video
Kajala ashangazwa na Anjella kumdhihaki kwenye video
Image: Instagram

Mwanamama Kajala Fridah ameendeleza mashambulizi yake kwa aliyekuwa mpenzi wake Harmonize ya hivi karibuni akigusia kuondoka kwa msanii wa kike Anjella katika lebo ya Kondo Music Worldwide inayomilikiwa na Harmonize.

Katika klipu moja ambayo imepakiwa na Wasafi Media YouTube, Kajala amezua madai mengine kwamba wakati Anjella anaondoka kwenye lebo hiyo, alifanya juu chini kumshawishi Harmonize kumuachia msanii huyo hata gari lakini Harmonize hakusikia la mwadhini wala la mteka maji msikitini.

Kajala alijitoa kwenye picha kuwa aliwahi mfanyia Anjella mabaya, kufuatia wengi kuhisi hivyo Anjella alivyoachia wimbo wake – Blessing – miezi michache iliyopita akiashiria kugusia makovu aliyotendwa na Konde Gang, pia akiashiria jinsi ushawishi wa Kajala kwa Harmonize ulivyomsukuma nje kabisa.

“Mimi mwenyewe nilishtuka sana nilivyoona hiyo video ya Anjella, kwa sababu nakumbuka hata ambavyo alikuwa anataka kuondoka mimi ndio mtu wa kwanza hata nilikuwa namwambia Harmo [Harmonize] Anjella ni mtu ambaye anaumwa yaani ikiwezekana muachie hata gari aende nalo, hata akisimama yeye mwenyewe aongee sasa hivi,” Kajala alisema.

Kajala alisema kama watu wengine, pia yeye video ya Anjella ilimshtua sana kuona jinsi Kajala na Harmonize feki kwenye video hiyo walivyoigiza, Kajala huyo wa michongo akionesha roho mbaya kwa Anjella katika scene moja alipofika kwenye chumba chao akitaka usaidizi kutoka kwa Harmonize.

“Nilivyoona ile video mwenyewe I was like… yaani sijui labda mtu mwenyewe unaona upepo unavyoenda na wewe unaamua kuufuata, kwa hiyo nikasema sawa tu,” Kajala aliongeza.

 Mitandaoni, Kajala na Harmonize wanazidi kuparurana baada ya Harmonize kusema mengi kwenye wimbo wake wa Dear Ex ambao moja kwa moja unatupa vijembe kwa Kajala jinsi alivyomfanya zuzu wakati wanachumbiana.