Harmonize ataja mafanikio yake ni kutokana na Wizkid, Davido, BurnaBoy... amtema Diamond

"...Hivi majuzi pia nilipata nafasi ya kujifunza mengi kutoka kwa Ruger kwenye jukwaa, nakupenda sana kaka,” Harmonize aliandika.

Muhtasari

• Harmonize anahisi wasanii wa Bongo wanaojaribu kujishindanisha na wasanii wa Nigeria wanajishobokesha bure.

Harmonize.
Harmonize.
Image: Instagram

Msanii wa kizazi kipya nchini Tanzania amesema kwamba yeye hakuna hata siku moja atakuja kuanza kujishindanisha na wasanii kutoka Taifa la Nigeria ambao wanafanya vizuri kimuziki katika bara la Afrika

Kupitia Instagram, Harmonize anahisi kwamba badala ya kushindana nao – ambao ni kama kushiriki mchezo wa pata potea – yeye ameamua kujifunza kutoka kwao, akisema kwamba kushindana nao si katka kizazi hiki bali ni katika kizazi kijacho, labda.

“Mimi niondoe kwenye orodha ya baadhi ya wasanii wa Tanzania ambao wanadhani tunaweza shindana au kuanzisha uhasama na wasanii wa Nigeria. Pengine katika kizazi kijacho tu,” Harmonize alisema.

Akitaja sababu ya kutojaribu hata siku moja kuanzisha uadui na wasanii wa Nigeria, Harmonize alisema kuwa anawaona wasanii wengi kutoka taifa hilo kama amabo wamechangia pakubwa kwenye ufanisi wake kimuziki, akiwataja baadhi kila mmoja na mchango wake katika maisha yake ya muziki.

“Ujasiri wangu umehimizwa na Wizkid, swag yangu imetokana na Burna Boy, jinsi ya kulinda muda nimejifunza kutoka kwa Davido na pamoja tunaweza tengeneza Afrobeats nzuri. Hivi majuzi pia nilipata nafasi ya kujifunza mengi kutoka kwa Ruger kwenye jukwaa, nakupenda sana kaka,” Harmonize aliandika.

Katika orodha ya wasanii hao waliompa mafanikio, msanii huyo hakumtaja Diamond kwenye wasanii waliomsaidia, licha ya kujulikana bayana kwamba ndiye alikitambuak ipaji chake na kumpa nafasi ya kumsaini kama msanii wake wa kwanza kabisa kwenye lebo ya WCB Wasafi.

Harmonize na Diamond wamekuwa wakihasimiana kwa takribani miaka mitatu sasa, tangu msanii huyo alipoondoka kwenye lebo ya Wasafi mwishoni mwa mwaka 2019.