Eric Omondi aongoza familia ya mtoto Pyden kuondoa mwili mochwari, kuusafirisha

Eric Omondi alichangisha takribani milioni moja mitandaoni kwa ajili ya matibabu ya mtoto huyo lakini alifariki muda mchache baada ya kumfikisha hospitalini. Jeneza la mtoto siku zote huwa zito sana!

Muhtasari

• Siku chache zilziopita, Eric Omondi aliongoza wafuasi wake kwenye mtandao wa Instagram kuchangisha hela.

Eric aliondoka na familia ya Mudoga.
Eric aliondoka na familia ya Mudoga.
Image: Instagram

Mwanaharakati wa haki za kibinadamu Eric Omondi ameongoza familia ya mtoto Pyden Mudoga katika shughuli moja nzito sana kwa mioyo ya wengi – kuondoa mwili wa mtoto huyo kutoka makafani tayari kuusafirisha kwa ajili ya maziko.

Kupitia Instagram, Omondi alipakia klipu fupi yenye uchungu mkubwa wakiondoa mwili huo kutoka chumba cha kuhifadhi maiti na kuupakiza kwenye gari la kubeba maiti tayari kwa safari kwenda makazi yake ya milele.

Omondi aliandika ujumbe wa hisia za kutia huruma akisema kwamba jeneza la mtoto siku zote huwa ni zito sana kwa mzazi wake kubeba na mzazi kumzika mtoto wake ni sawa na kuizika sehemu ya nafsi yake.

“Wanasema Jeneza ndogo ni nzito zaidi. Safiri salama Pyden Mudoga. Mengi yanahitaji kubadilika katika mifumo yetu ya afya. Tulifika Pyden kwa kuchelewa kidogo lakini wiki ijayo tutakuwa tukizindua kitu ambacho kitabadilisha maisha ya watu. Mahali imefika sasa lazima itakua ni #SisiKwaSisi,” Eric Omondi alitoa kauli hiyo ya kiharakati.

Siku chache zilziopita, Eric Omondi aliongoza wafuasi wake kwenye mtandao wa Instagram kuchangisha hela kwa ajili ya matibabu ya mtoto huyo ambaye walikuwa wanaishi mtaa duni wa Kawangware.

Ndani ya saa chache, Omondi alidokeza kwamba watu walioguswa na huruma kutokana na hali ya mtoto yule waliweza kuchangiza takribani shilingi milioni moja lakini kwa bahati mbaya mtoto huyo alifariki baada ya kufikishwa hospitalini siku moja baadae.