Zuchu kumshtaki Mwijaku kisa kujibizana na mamake kuhusu kuzini kwa mwanawe

"Wallahi naapa nitatumia kila senti kwenye akaunti yangu na wallahi nitakutolea mfano, nimekuacha mno ila kwa hili la mamangu utakuwa fundisho kwa wenzio,” Zuchu alikula yamini.

Muhtasari

• Hata hivyo, Mwijaku alionekana kuingiza tumbo maji na kunywea kwa kumwambia Zuchu kwamba si yeye alimzungumzia mamake.

Zuchu na Mwijaku
Zuchu na Mwijaku
Image: insta

Sa chache baada ya Mwijaku kuchafuana vikali katika mtandao wa Instagram na Khadija Kopa, mamake Zuchu, msanii huyo wa WCB Wasafi ameingilia kati na kuapa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtangazaji Mwijaku kisa kumdhalilisha mamake bayana machoni pa watu mitandaoni.

Mwijaku alipakia klipu kutoka kwa mahojaino baada ya kuramba ubalozi na kusema kwamba amejaribu kadri ya uwezo wake kumshauri Zuchu kukoma kuzini na Diamond akisema kuwa bosi huyo wa WCB anamtumia tu kisha ambwage.

Mwijaku alisema kuwa hata mamake Zuchu mwenyewe anaonekena kulitukuza suala la Zuchu kuzini na Diamond kabla ya ndoa, akisema kuwa ni kinyume na matakwa ya Allah.

Mwijaku alikwenda hatua Zaidi na kunukuu aya kadhaa za msahafu akisema kuwa  ni vibaya mtu kuzini kabla ya ndoa – suala ambalo alisema Khadija Kopa anaonekana kulifurahia licha ya kwamba ni muislamu.

Wawili hao walijibizana na kuchafuana kwa maneno kiasi kwamab suala hilo limemuuma sana Zuchu na kukiri kwamba hawezi kukaa pembeni akiona mamake akidhalilishwa kisa yeye.

Ameapa kuelekea katika mkondo wa kisheria kutumia hata kama ni pesa zake zote lakini kuhakikisha mama yake anapata heshima ambayo anastahili.

“Kwenu hakuna wazinzi? Hujamaliza kuzungumza nao hao mpaka ukamuongelelee mamangu kwenye vyombo vya habari. Wallahi naapa nitatumia kila senti kwenye akaunti yangu na wallahi nitakutolea mfano. Zungumza kabisa na mabosi wako wanaokuweka na mimi nitazungumza na huyo unayesema sisi tumfuate wallahi nimekuacha mno ila kwa hili la mamangu utakuwa fundisho kwa wenzio,” Zuchu alikula yamini.

Hata hivyo, Mwijaku alionekana kuingiza tumbo maji na kunywea kwa kumwambia Zuchu kwamba si yeye alimzungumzia mamake bali mamake ndiye aliyeanza kumzungumzia akimuita majina ya fedheha.

“Mie sijamuongelea mama yako. Yeye ndiye kanifuata na kuniita jina Kipwite. Jiulize nani kamfuata mweziwe. Na hapo nimekumbusha tu kwa sababu ni wajibu wangu kama muislamu,” Mwijaku alijitetea mbele ya Zuchu aliyechemka.