Ringtone aorodhesha masharti Bahati anafaa kutimiza ili kukaribishwa kwenye injili tena

"Mungu kama amemuita Bahati anafaa kufuta kila kitu ikiwemo chaneli na kurasa za mitandaoni. Aanze upya, Mungu atampa tena, atampa watu wapya." - Ringtone.

Muhtasari

• Ringtone alisema kuwa Bahati ameonesha picha mbaya sana haswa picha za hivi majuzi akivuta kile kilichokisiwa kuwa Bangi.

• Msanii huyo alitetea msimamo huo akisema kuwa Bahati kurejea kwa injili itakuwa sawa sawa na kubatizwa upya ili kutakaswa.

Ringtone na Bahati
Ringtone na Bahati
Image: Instagram

Wikendi iliyopita baada ya mchungaji Lucy Natasha kufanya ibada ya kumuombea msanii Bahati Kioko ili kurudi katika muziki wa injili, msanii anayejiita mwenyekiti wa wainjilisti Ringtone Apoko ametoa maoni yake.

Akifanya mahojiano na Mungai Eve, Ringtone alisema kuwa japo katika Biblia msamaha unahimizwa, yeye kama mwenyekiti wa Sanaa ya injili Kenya hayuko tayari kumkubali Bahati kurudi kwenye injili.

Ringtone alisema kuwa Bahati ameonesha picha mbaya sana haswa picha za hivi majuzi akivuta kile kilichokisiwa kuwa Bangi.

Msanii huyo mwenye mikogo alitaja baadhi ya masharti ambayo itamlazimu Bahati kuyatekeleza iwapo anataka kukubaliwa kurejea katika Sanaa ya injili ambayo aliitelekeza miaka kadhaa iliyopita na kuhamia miziki ya kidunia.

“Bahati atumkati kurudi kwenye injili mpaka afanye vitu kadhaa, cha kwanza akane muzki wa sekula, video zote zile amefanya afute kabisa – unajua huwezi kuwekeza kwa Mungu ukitumia vitu vya kishetani. Mungu kama amemuita Bahati anafaa kufuta kila kitu ikiwemo chaneli na kurasa za mitandaoni. Aanze upya, Mungu atampa tena, atampa watu wapya. Akifuta atapata watu wengine watakaomfuata kwa hiyo safari mpya,” Ringtone alisema.

Msanii huyo alitetea msimamo huo akisema kuwa Bahati kurejea kwa injili itakuwa sawa sawa na kubatizwa upya ili kutakaswa.

“Sababu ya mtu kubatizwa kibibilia tunasema anazikwa na anazaliwa upya. Bahati lazima azike vitu vyote vya kidunia, hizo nyimbo mbaya zilizofanya watu wengi kwenda jehanamu, afute… nyimbo za Bahati iznafanya watu wengi sana wanapenda ulevi na usherati, kwa hiyo lazima azifute zote kama ameaua kuacha mambo ya kishetani,” aliongeza Ringtone.

Msanii huyo alikwenda mbele Zaidi na kusisitiza kwamba Bahati anafaa kuachia kila kitu ambacho alipata kutokana na muziki wa kidunia ikiwemo magari, mavazi ambayo amewahi yavaa kwenye video za miziki yake ya sekula, apatiane bure ili arudi kwa Mungu akiwa bila kitu.

“Apeane kila kitu akuje kwa Mungu, Mungu amjenge upya na kumtumia. Bila hivyo ni kazi bure, Mungu hawzi kubali dhabihu ya uimbaji wake,” alisema.