Tunaongelesha WaTZ kwa Kiswahili kibaya, wanatujibu kwa kizungu kibaya - Larry Madowo

Kwa kauli hii ya Larry Madowo, watu mitandaoni walisema kwamba mchezo wa ubabe wa lugha hizo mbili baina ya KE na TZ ulienda draw.

Muhtasari

• Samia alisema kwamba Ruto aliwaambia wajumbe wa kimataifa kwamba salamu ni “jambo” hali ya kuwa alifaa kuwaambia waseme “habari za mchana”.

• Kiongozi huyo mtetezi wa Kiswahili alisema kwamba Wakenya wanaharibu Kiswahili na wanahitaji kurudishwa darasani.

Larry Madowo amtetea Ruto kisa Kiswahii
Larry Madowo amtetea Ruto kisa Kiswahii
Image: Maktaba

Kwa mara nyingine tena mwanahabari wa kimataifa wa CNN kutoka nchini Kenya, Larry Madowo amezua mjadala mkali mitandaoni kuhusu mataifa jirani Kenya na Tanzania kuhusu weledi wa lugha za Kiswahili na Kiingereza.

Madowo ambaye alikuwa katika mkutano wa chakula nchini Tanzania pamoja na rais wa Kenya William Ruto alizungumza kwa kumtetea Ruto baada ya rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kudai kwamba Ruto aliboronga Kiswahili wakati wa mkutano wa kilele wa mabadiliko ya hali ya hewa jijini Nairobi mwanzoni mwa wiki.

Samia alisema kwamba Ruto aliwaambia wajumbe wa kimataifa kwamba salamu ni “jambo” hali ya kuwa alifaa kuwaambia waseme “habari za mchana”.

Kiongozi huyo mtetezi wa Kiswahili alisema kwamba Wakenya wanaharibu Kiswahili na wanahitaji kurudishwa darasani.

Hata hivyo, Madowo alimtetea Ruto akisema kwamab hata Watanzania huwa wanazungumza na Wakenya kwa Kiingereza kilichobanangwa na wao [Wakenya] huwajibu kwa Kiswahili kisicho sahihi na maisha yanaendelea mbele kama injili.

”Lazima nitetee Rais wangu Ruto kwa sababu najua sisi wakenya na watanzania, sisi ni mandugu wa karibu. Tunaongelesha waTanzania kwa Kiswahili kibaya, wanatujibu na kizungu kibaya, tunasonga mbele Kama injili,” alisema.

Aliongeza kuwa hakuna zaidi ya kuzungumza juu ya hilo kwani ni suala la familia.

Rais William Ruto kwa upande wake alibainisha kuwa Kiswahili chake ni bora kuliko Larry Madowo. Pia ameachwa na mwenzake wa Tanzania, Samia Suluhu, akicheka kicheko baada ya kushiriki vichekesho vya kuchekesha kuhusu Azimio la Umoja One Kenya Coalition.

“Nimesikia ukitaja Azimio, Azimio, Azimio, mpaka nikapata wasiwasi kidogo. Kwa sababu katika nchi yetu, Azimio ina maana tofauti. Kwa upande wetu, Azimio ni chama cha upinzani ambacho kinaamini katika machafuko mengi,” Ruto alisema.