Karen Nyamu aungana na mpenziwe Samidoh jukwaani Australia kutumbuiza - Video

Nyamu alionyesha mtindo wake wa kucheza kwa kuzunguka huku Samidoh akishindwa kujizuia kwa tabasamu pana akicheza gitaa na kando yake mpenzi wake anacheza kwa furaha.

Muhtasari

• Bila shaka, Karen Nyamu ndiye shabiki namba moja kwa muziki wa Samidoh, hata wakati hakuna mtu mwingine anayemuunga mkono, Nyamu atakuwepo.

Samidoh na mpenziwe Karen Nyamu
Samidoh na mpenziwe Karen Nyamu
Image: Maktaba

Msanii wa mugithi Samidoh yuko nchini Australia kwa msururu wa kutumbiza na sasa imebainika kwamba mpenzi wake Karen Nyamu alimfuata kule siku chache zilizopita.

Itakumbukwa awali tuliripoti kwamba Nyamu alipakia picha akiwa katika uwanja wa ndege jijini Dubai ambako aghalabu ndege za Kwenda Australia kutoka Kenya hupitia katika mataifa ya Uarabuni kabla ya kuunganisha moja kwa moja kwenda Australia.

Katika video ambayo imeibuka mitandaoni, Karen Nyamu alionekana kuungana na mpenzi wake Samidoh katika jukwaa moja na kutumbuiza pamoja huku mashabiki wao wakifurahia ajabu.

Katika video hiyo, seneta huyo maalum, ambaye alikuwa amevalia nguo fupi ya rangi nyeusi iliyokumbatia mwili na viatu vyekundu, aliungana na mwimbaji Mugithi jukwaani, naye akaimba moja ya nyimbo zake maarufu huku akicheza.

Mama huyo wa watoto watatu alionyesha minenguo yake huku umati ukishangilia kwa nguvu. Nyamu alionyesha mtindo wake wa kucheza kwa kuzunguka huku Samidoh akishindwa kujizuia kwa tabasamu pana akicheza gitaa na kando yake mpenzi wake anacheza kwa furaha.

Mashabiki wa mwanasiasa huyo walimshabiki wakisema kwamba wanapenda jinsi anavyokuja katika mstari wa mbele kuonesha kuunga mkono kile ambacho mpenzi wake anafanya kutafuta riziki.

Bila shaka, Karen Nyamu ndiye shabiki namba moja kwa muziki wa Samidoh, hata wakati hakuna mtu mwingine anayemuunga mkono, Nyamu atakuwepo.

Tazama video hii hapa chini jinsi Nyamu aliwakosha mashabiki waliohudhuria tamasha hilo kwa minenguo ya kibabe.