Khaligraph adai Diamond aliiga wazo lake kuingia jukwaani akiwa ndani ya jeneza

"Mimi niliingia jukwaani nikiwa ndani ya jeneza miaka 6 iliyopita, ni lazima OGs wapewe heshima," Khaligraph aliandika kwenye video hiyo ya Koroga Festival mwaka 2017.

Muhtasari

• Sasa Khaligraph amemchokoza akisema kwamba ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuja na wazo hilo, huku akisema kuwa OGs siku zote watabaki kuheshimiwa na si vingine.

• Japo baadae katika chapisho kwenye X, awali ikiwa ni Twitter, Diamond alikiri kuingiwa na woga alipokuwa ndani ya jeneza.

Diamond Platnumz na Khaligraph Jonez wazozana kisa kuingia ukumbini na jeneza.
Diamond Platnumz na Khaligraph Jonez wazozana kisa kuingia ukumbini na jeneza.
Image: Instagram, X

Tukio la Diamond Platnumz kuingia jukwaani akiwa amebebwa ndani ya jeneza usiku wa Jumamosi katika tamasha la Wasafi linaendelea kuvutia maoni mbali mbali.

Mtu wa hivi punde kutoa maoni yake kwa uchokozi ni msanii kutoka Kenya, rapa Khaligraph Jones ambaye alitupa dongo wa Diamond akiashiria kwamba Diamond aliiga wazo lake la kuingia kwenye jukwaa akiwa ndani ya Jeneza.

Kwa kumbukumbu tu, Khaligraph Jones aligonga vichwa vya habari Desemba ya 2017 baada ya kuingia kwenye jukwaa la tamasha la Koroga akiwa amebebwa ndani ya jeneza.

Msanii huyo baada ya jeneza lililokuwa limebebwa na takriban wanaume 8 waliounga misuli kutua jeneza jukwaani, alitoka ndani huku akiwa amejihami na kipaza sauti mkononi na kuanza kutumbuiza kabla ya watu kuvuta picha kuona kama kweli ni yeye ama ni maiti iliyofufuka.

Diamond alionekana kufanya maigizo kama hayo katika shoo ya Wasafi Festival mkoani Lindi ambapo pia alibebwa akiwa ndani ya jeneza kabla pia ya kuchomoka ndani akitumbuiza moja kwa moja.

Japo baadae katika chapisho kwenye X, awali ikiwa ni Twitter, Diamond alikiri kuingiwa na woga alipokuwa ndani ya jeneza.

Sasa Khaligraph amemchokoza akisema kwamba ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuja na wazo hilo, huku akisema kuwa OGs siku zote watabaki kuheshimiwa na si vingine.

“Miaka 6 iliyopita, OG lazima aheshimiwe,” Khaligraph aliandika huku akiambatanisha na video fupi ikirudisha kumbukumbu za jinsi aliingia jukwaani kwenye jeneza katika tamasha la Koroga mwaka 2017.

Hili linakuja kama mwendelezo wa mashambulizi ya kutaniani ambayo yalianzishwa na Jones wiki chache zilizopita aliposema kwamba muziki wa rap nchini Tanzania umepoteza maana kabisa.

Khaligraph katika wimbo wake wa kuwazomea Watanzania aliwapa marapa wa nchi hiyo jirani muda wa saa 24 kumjibu la sivyo atachukua kiti kama mfalme wa Rap nchini humo, miaka michache baada ya kujidai kwamba ameiteka Nigeria na kutawazwa kama rapa namba moja katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu Afrika.